Na Muhidin Amri,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imedhamiria
kuhakikisha kwamba inaongeza kasi juu ya suala la usafi wa mazingira katika
Manispaa hiyo ambapo imejiwekea mkakati wa kununua kijiko kimoja cha kuzolea
taka, kwa shilingi milioni 170 ili kuweza kurahisisha kazi ya uzoaji taka
kwenye maeneo mbalimbali.
Ofisi za halmashauri ya mji wa Songea. |
Aidha katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imeweza kutenga fedha
hizo ambazo watahakikisha kifaa hicho kinanunuliwa mapema, kwa lengo la
kuufanya mji wa Songea uendelee kuwa safi wakati wote.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na
Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa pamoja na kuweka
mikakati hiyo pia wamekuwa wakihamasisha wananchi kutokiuka kanuni na sheria za
afya zilizowekwa ambazo zinaifanya jamii iendelee kuishi bila kushambuliwa na
magonjwa ya mlipuko kutokana na kuzingatia masuala ya usafi.
Midelo alieleza kuwa Manispaa ya Songea imekuwa ikizalisha taka
tani 155 kwa siku ambazo zinatoka kwenye majengo ya biashara, taasisi
mbalimbali, viwanda vidogo vidogo, vituo vya kutolea huduma za afya na nyumba
za kuishi.
Alifafanua kuwa halmashauri hiyo ina magari matatu ya
kuzolea taka hizo ngumu ambapo magari hayo yanauwezo wa kuzoa tani 94.24 ya lengo
la kuzoa tani 124 kwa siku sawa na asilimia 76.
“Manispaa hii pia inatarajia kuunda vikundi vya askari wa kupita
kusimamia masuala ya usafi wa mazingira, ambao watasaidia kusimamia usafi
katika mitaa yote 95 iliyopo ndani ya Manispaa hii”, alisema.
Vilevile Midelo alieleza kuwa mpango wa kuanzisha vikundi
hivyo, unaendelea vizuri ambapo tayari kata tano kati ya 21 wamekwisha wasilisha
majina ya vijana ambao wameomba kufanya kazi hiyo.
Kadhalika uongozi husika wa Manispaa umeamua kutumia
vikundi vya askari hao ili kuweza kusimamia kikamilifu shughuli za usafi wa mazingira
na kuhakikisha kwamba hakuna mtu ambaye ataweza kuchafua mazingira hayo bila
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema tayari baraza la Madiwani la Manispaa ya Songea limeunga
mkono na kuidhinisha shughuli za usafi wa mazingira ndani ya halmashauri hiyo zifanywe
kwa kutumia vikundi vya askari wa usafi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment