Monday, January 30, 2017

WANAFUNZI NYASA WANUSURIKA KIFO BAADA YA KUJERUHIWA NA RADI

Na Kassian Nyandindi,       
Nyasa.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wanafunzi wanaosoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Unberkant wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma wamenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na radi wakati wakiwa darasani, huku mfumo wa njia za umeme uliopo shuleni hapo ukiwa umeharibiwa vibaya.

Wanafunzi hao walikuwa 25 na kwamba Mkuu wa shule hiyo, Stephen Mwela naye amejeruhiwa bega la kushoto ambapo alisema kuwa tukio hilo lilianzia katika Ofisi ya mkuu huyo wa shule kwa kupiga radi ukutani ambako ndiko kwenye mfumo wa umeme ambao unatumika shuleni hapo.

Akifafanua juu ya tukio hilo mbele ya Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge mkuu huyo wa shule ya sekondari Unberkant, Mwela alisema kuwa baada ya kuharibu mfumo huo wa umeme radi hiyo ilisambaa katika maeneo mengine ya shule hadi darasani walikokuwa wanafunzi hao na kuwajeruhi.

“Wanafunzi watatu wana hali mbaya, wawili wamelazwa Kituo cha afya Mbamba bay na mwingine mmoja tumelazimika kumpeleka hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho kwa ajili ya matibabu zaidi”, alisema Mwela.


Aliongeza kuwa tukio hilo lilitokea Januari 22 mwaka huu majira ya asubuhi wakati watoto hao wakiwa darasani wanasoma, hata hivyo wanafunzi 22 tayari wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kwenda shuleni hapo kuendelea na masomo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Esabela Chilumba alisema kuwa kwa kawaida wilaya hiyo imekuwa na matukio ya radi mara kwa mara kutokana na uwepo wa ziwa Nyasa lililozungukwa na milima ndiyo sababu kuu inayoifanya jamii iweze kuathirika na hali hiyo.

Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge ambaye alitembelea shule hiyo mbali na kuwapa pole wanafunzi na walimu hao alisema kuwa hilo ni tukio la kisayansi hivyo aliwataka wanafunzi kuwa wavumilivu na kuweza kuendelea na vipindi vyao vya masomo darasani.

Alisema kuwa watu wengine tukio hilo wanalihusisha na mambo ya ushirikina ambapo amewataka kuachana na imani hizo potofu, badala yake wakati umefika kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuachana na mambo hayo bali waongeze juhudi ya kuwapatia watoto wao elimu ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Dkt. Mahenge aliwataka wauguzi na madaktari kuhakikisha kwamba wanakuwa karibu na majeruhi hao kwa kuwapatia huduma muhimu za matibabu ili waweze kupona haraka na kuendelea na masomo yao.

Mbali na hilo Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma ametoa rai kwa  uongozi wa shule na wananchi   wa Nyasa, kuchukua tahadhari mara wanapoona mingurumo ya radi kwa kuzima radio, simu na vifaa vingine vinavyotumia umeme ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kutokea hapo baadaye.


Dkt. Mahenge amemuagiza pia Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa kuhakikisha kwamba anatafuta fedha haraka, ili kurudisha mfumo wa umeme katika shule hiyo na wanafunzi wapate fursa ya kujisomea vizuri hasa nyakati za usiku.

No comments: