Na Mwandishi wetu,
Songea.
ZAIDI ya watu 21,000 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
wamebainika kuishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hivyo wananchi wamesisitizwa kutunza
afya zao ili kuweza kuepukana na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi,
utakanao na virusi hivyo.
Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa takwimu
hizo zimetolewa na kitengo cha uratibu wa Ukimwi na tiba katika Manispaa ya
Songea ambapo inaonesha kuwa kati ya watu wenye virusi hivyo, zaidi ya 10,000
ndiyo ambao wanaugua ugonjwa wa Ukimwi.
Alisema kuwa idadi hiyo ni wale wanaotumia dawa za kurefusha
maisha (ARV) na kwamba maambukizi ya virusi hivyo yamefikia asilimia nne.
Midelo amezitaja kata ambazo zinaongoza kwa maambukizo ya ugonjwa
huo katika Manispaa ya Songea kuwa ni Bombambili, Mateka, Ruvuma na Lilambo.
Alifafanua kuwa takwimu za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU)
katika Manispaa hiyo kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Disemba mwaka jana zinaonesha
kuwa watu 319 wamegundulika kuwa na maambukizi mapya ya virusi hivyo.
“Kati ya waliogundulika wanaume ni 114 na wanawake ni 205
sawa na asilimia 4.2 ya watu waliopima ambao ni 7,510, kati ya hao wanaume
3,417 na wanawake 4,093 na takwimu zinaonesha kuwa maambukizi ya virusi hivi katika
makundi maalum yamefikia asilimia 36 ambapo kila watu 100 watu 36 wana Virusi
vya Ukimwi ukilinganisha na kiwango cha kitaifa cha asilimia tano ambayo ni
sawa na kila watu 100 watano wanaishi na virusi vya ugonjwa huu”, alisema.
Katika kupambana na hali hiyo alisema kuwa Manispaa imeweka
mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa janga hilo la Ukimwi linapungua, kwa kushirikiana
na wadau wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma.
Ofisa habari huyo ameitaja mikakati inayoendelea kufanywa
hadi sasa katika kukabiliana na ugonjwa huo kuwa ni uzuiaji wa maambukizi
kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (PMTCT), upimaji wa hiari (VTC), upimaji wa
kila mteja anayefika katika vituo vya huduma (PITC), huduma ya wagonjwa wenye
magonjwa nyemelezi na uanzishwaji wa vikundi vya wenye kuishi na Virusi vya Ukimwi.
Manispaa ya Songea ina Vituo 24 vya kutolea huduma ya dawa za
kupunguza makali ya Ukimwi (CTC) na dawa zinatolewa bila malipo kwa wagonjwa wenye
ugonjwa huo na kwamba kuna vituo 26 ambavyo hutoa huduma za kuzuia maakumbukizi
ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma ya wagonjwa majumbani kwa
wenye magonjwa sugu, hivyo vituo vimeongezeka kutoka 17 na kufikia 20.
Hata hivyo mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tano kitaifa
ukiwa na maambukizi ya asilimia saba, ambapo mkoa wa Njombe ndiyo unaongoza
kitaifa ukiwa na asilimia 14.5 nafasi ya pili inashikwa na mkoa wa Iringa,
ikifuatiwa na mkoa wa Mbeya kwa nafasi ya tatu na mkoa wa Rukwa ukiwa nafasi ya
tano.
No comments:
Post a Comment