Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)
Mlingi Mkucha amejikuta akiwa katika wakati mgumu baada ya kushindwa kutolea
ufafanuzi mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juu ya kodi ya gawio la
serikali inayopatikana katika mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji
cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Aidha kufuatia hali hiyo, serikali hapa nchini imesema kuwa
itamtuma Gavana wake wa Benki kuu pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) kwenda kufuatilia mwenendo mzima wa fedha za kodi ya serikali
katika mgodi huo, ili kuweza kujiridhisha kama kodi hiyo ilikuwa inalipwa
serikalini ipasavyo au la.
Hayo yalijitokeza jana mbele ya Waziri Mkuu, Majaliwa alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa, baada ya kutembelea mgodi huo kwa
lengo la kujionea maendeleo yake na changamoto mbalimbali zilizopo ambapo
alisema kuwa endapo ukweli ukibainika baada ya ukaguzi kufanyika, wahusika
walioshiriki kukwepa kulipa kodi hiyo watawajibika kulipa tangu mgodi huo
ulipoanza.
Waziri Mkuu Majaliwa alifafanua kuwa kuna harufu ya ufisadi
juu ya fedha hizo za serikali ambapo tokea mgodi huo uanzishwe mwezi Julai
mwaka 2011 serikali imekuwa haipati gawio lake la kodi ipasavyo, hivyo ameagiza
ukaguzi ufanyike haraka ili kuweza kujiridhisha fedha hizo zilizokuwa
zikipatikana kutokana na mauzo ya makaa ya mawe zilikuwa zikipelekwa wapi.
“Nimegundua nyie mmeamua kubana mianya ya serikali kupata
fedha zake, kama hamtaweza kusimamia hili NDC tutamweka mtu ambaye atasimamia
jambo hili ili serikali iweze kupata fedha zake, haiwezekani mnaendelea
kuzalisha malighafi halafu serikali bado inapata hasara”, alisema.
Alisema kuwa mgodi wa Ngaka ni mgodi ambao unatoa makaa ya mawe
yenye viwango vya ubora wa hali ya juu katika bara la Afrika, hivyo una kila
sababu ya kuwanufaisha Watanzania wenyewe na sio vinginevyo.
Vilevile aliongeza kuwa atamtuma Mwanasheria mkuu wa serikali
apitie mikataba yote ya mgodi huo kwani inaonesha kuna utata mkubwa ambao
unaisababishia serikali kukosa fedha zake za gawio la kila mwaka la kodi
itokanayo na mauzo ya makaa hayo na kusababisha iendelee kupata hasara.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kukusanya
kodi kikamilifu sambamba na kupitia mikataba yote ya makampuni
yanayojishughulisha na uchimbaji wa madini hapa nchini, ili kuona namna gani
nchi inanufaika na rasilimali zake.
Majaliwa aliongeza kuwa ni vyema shirika la NDC likawa makini
katika kuhakikisha kwamba linaisimamia ipasavyo kampuni ya TANCOAL Energy
inayochimba makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka, uliopo kata ya Ruanda wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma ikiwa ni pamoja na kulipa mapato ya serikali kama
inavyotakiwa.
Katika hatua nyingine akizungumza na wananchi wa kata hiyo
Waziri Mkuu huyo aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inatekeleza jukumu lake la
kupeleka maji safi na salama katika maeneo wanaoishi wananchi waliopo karibu na
mgodi, sambamba na kusaidia kuboresha miundombinu ya shule za msingi kama
walivyokubaliana katika mikataba husika.
Vilevile alimuagiza Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini,
Martin Msuha kufuatilia masuala hayo yanayotakiwa kutekelezwa na kampuni hiyo
kwa wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na kuondoa malalamiko yasiyokuwa
ya lazima.
Alisisitiza pia juu ya umuhimu wa kampuni hiyo kujenga
barabara ya kutoka Kitai hadi mgodini kwa kiwango cha lami, ili kuwaondolea
adha wananchi kupata vumbi linatokana na makaa hayo wakati yanaposafirishwa
kutoka mgodini kwenda kwa wateja.
No comments:
Post a Comment