Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ASKOFU Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo kuu la Songea mkoani
Ruvuma, Damian Dallu amewataka viongozi hapa nchini kutumia hekima na busara
katika kuliongoza taifa, kwa lengo la kuwatendea haki wananchi wanaowaongoza
kwa ajili ya kudumisha amani na mshikamano.
Dallu aliyasema hayo juzi alipokuwa akihubiri katika
ibada ya misa takatifu ya mkesha wa kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya
wa 2017 iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba
mjini Songea.
Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea, Damian Dallu. |
Alisema kuwa baadhi ya mataifa yameingia katika machafuko
kutokana na viongozi wake kushindwa kutumia hekima na busara, katika kutatua
changamoto na migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi wake wanaowaongoza.
Kadhalika Askofu huyo amewataka viongozi hao kutumia mwaka
mpya wa 2017 katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa hili,
ikiwemo migogoro ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji ambayo inasababisha umwagaji
wa damu katika baadhi ya maeneo pale inapotokea.
Vilevile kiongozi huyo wa dini amekemea tabia inayofanywa na
baadhi ya wananchi ya kukata viungo vya watu wenye matatizo ya ngozi (Albino)
kwa imani kuwa vinaweza kuwasaidia kupata utajiri, pamoja na vyeo mbalimbali
vya kisiasa jambo ambalo ameliita kuwa ni imani potofu na badala yake amewataka
wawe na hofu ya Mungu.
Aidha amewataka waumini hao kuutumia mwaka huu katika
kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kumuomba Mungu ili aweze kuwajalia mafanikio
mbalimbali ikiwemo hekima, afya njema, ulinzi na usalama, baraka za kimwili na
kiroho kama ilivyokuwa kwa wana wa Israel.
Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa waumini wengi hivi sasa
wameyumbishwa kiimani, kutokana na kukabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo
kutetereka kiafya na kwamba amewatahadharisha waumini hao kujiepusha pia na
matapeli ambao wanapitia kwa mgongo wa dini.
No comments:
Post a Comment