Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa kesho anatarajia kuanza ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani
Ruvuma ambapo atapata fursa ya kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo ya
wananchi, katika wilaya ya Mbinga na Songea mkoani hapa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa mkoa huo,
Dkt. Binilith Mahenge alisema kwamba Majaliwa atawasili katika uwanja wa ndege
Songea majira ya saa 9.00 alasiri na kupokelewa na viongozi wa serikali na
chama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Aliwataka wananchi wote kwenye maeneo ambayo Waziri huyo
atafanya mikutano, wahudhurie kwa wingi ili kumsikiliza na hatimaye kutekeleza
maagizo yake ambayo atayatoa kwa viongozi, watendaji na wananchi kupitia
mikutano hiyo.
Dkt. Mahenge alisema kuwa mara baada ya kuwasili ataelekea
Ikulu ndogo iliyopo mjini hapa, ambako atapokea taarifa ya maendeleo ya mkoa na
kwamba baada ya hapo atazungumza na watumishi wa umma.
Alisema kuwa Januari 5 mwaka huu Waziri mkuu atatembelea
katika halmashauri ya Songea vijijini Madaba ambapo atazungumza pia na
watumishi wa serikali, kukagua na kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha
Magingo na baadaye atahutubia mkutano wa hadhara wananchi wa Madaba.
Dkt. Mahenge alifafanua kuwa Januari 6 mwaka huu, Majaliwa atatembelea
na kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe kwenye mgodi wa
Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga.
Alisema kuwa atakapokuwa kwenye kata hiyo atazungumza na
wananchi kupitia mkutano wa hadhara na kwamba Januari 8 mwaka huu atahitimisha
ziara yake kwa kufanya kikao cha majumuisho Ikulu ndogo mjini Songea na kurejea
jijini Dar es salaam.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi wa mkoa
wa Ruvuma kuhakikisha kwamba wanapanda kwa wingi mazao yanayostahimili ukame
kutokana na kutonyesha mvua ya kutosha kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma, na
kwamba wajiwekee chakula cha kutosha ili waweze kukabiliana na uwezekano wa
kutokea njaa.
Pia Dkt. Mahenge alisisitiza juu ya umuhimu wa kutunza
mazingira kwa kuacha kukata na kuchoma moto misitu au kuchoma mkaa jambo ambalo
limekuwa likisababisha kutokea kwa mabadiliko ya tabia nchi, kama Afrika na
dunia kwa ujumla wake.
No comments:
Post a Comment