Friday, January 20, 2017

MARTIN MSUHA NA MTAZAMO WA KUIJENGA UPYA MBINGA VIJIJINI

Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Martin Msuha akizungumza na wananchi wa kata ya Maguu na Mbuji juu ya mpango wa serikali unaowataka wakubali kupima maeneo yao ili waweze kuwa na hati miliki na kuweza kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima katika jamii, Msuha alikuwa katika ziara yake ya kikazi ya kuwatembelea wananchi wa jimbo hilo kwa lengo la kuhamasisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.  (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

NOVEMBA 5 mwaka jana Rais Dkt. John Magufuli ametimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, alipochaguliwa kushika wadhifa huo baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 ambao pia ulivishirikisha vyama mbalimbali vya upinzani.

Kama inavyofahamika wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita Rais huyo aliahidi masuala ambayo angeyatekeleza mara tu baada ya Watanzania kukipatia ridhaa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuongoza nchi, ambapo mpaka anatimiza mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani amefanikiwa kutimiza ahadi zake kwa asilimia kubwa na hivyo kuwafanya wananchi kuendelea kujenga imani kwa kiongozi huyo.

Wakati Watanzania hao wakishuhudia utendaji kazi wa kizalendo ambao umekuwa ukiendelea kutekelezwa na Dkt. Magufuli, Wabunge nao kwa upande wao wanapaswa kujitathimini na kueleza nini hasa wamewafanyia wananchi wao  waliowachagua tangu walipoingia madarakani mara baada ya uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba 25 mwaka 2015.

Ikumbukwe kwamba ushindi huo wa CCM ulitokana na Watanzania hawa kuwa na imani kubwa na chama hicho, hivyo kinachotakiwa sasa kwa viongozi wake ni kuendelea kutekeleza kwa vitendo yale yote ambayo yameainishwa ndani ya Ilani ya uchaguzi huo sambamba na yale ambayo waliahidi wao binafsi.

Katika uchaguzi huo mkuu ambao wabunge, madiwani na Rais walichaguliwa zipo pia ahadi mbalimbali zilitolewa kwa madai kwamba wangezitekeleza mara tu wakichaguliwa na kuingia madarakani, sasa ni vyema kila baada ya kipindi fulani viongozi hao ni muhimu wakayatafakari yale yote ambayo wameyafanya ili wananchi waweze kuyafahamu.

Katika makala haya, mmoja kati ya Wabunge ambao walitoa ahadi kwa wananchi wakati wa kuomba ridhaa ya kushika nafasi hiyo ya uwakilishi wa kuongoza wananchi, Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Martin Msuha ambaye alipeperusha bendera ya CCM na kuonekana kuwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho mara baada ya uchaguzi huo kufanyika.


Msuha alipohojiwa na waandishi wa habari anafafanua yale yote ambayo amefanikiwa kuyatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani kushika nafasi hiyo ya ubunge, ambapo anaeleza kuwa siri kubwa ya kufanikiwa kwake ni uwepo wa ushirikiano wa dhati baina yake na wananchi wa jimbo hilo.

Msuha anabainisha kuwa ushirikiano mzuri uliopo kati yake na viongozi mbalimbali, watendaji wa halmashauri na madiwani ndio hasa chanzo kikubwa cha kuyafikia mafanikio husika yaliyopo katika kila sekta ikiwemo elimu, afya, kilimo, barabara, maji, utunzaji wa mazingira na hata nishati ya umeme.

Akizungumzia juu ya kilimo anasema wananchi wa jimbo la Mbinga vijijini mkoani hapa kwa asilimia kubwa ni wakulima ambao hutegemea kilimo, ikiwa ndio njia kuu ya kujipatia kipato ambapo baadhi yao huzalisha mazao ya chakula kama vile mahindi, maharage, alizeti, ufuta na ulezi huku wengine wakijikita zaidi katika kilimo cha kahawa kama ndio zao kuu la biashara.

Anafafanua kuwa uzalishaji wa mazao haya kwa umoja wake wakulima wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kusababisha wakati mwingine kuporomoka kwa uzalishaji wake, ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kuishawishi serikali iendelee kutoa pembejeo za ruzuku ambazo kimsingi ni mkombozi mkubwa kwa wakulima hasa wadogo wadogo.

Mbunge huyo anaeleza kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja sasa anaendelea kushirikiana na wanachama wa Chama kikuu cha ushirika cha MBIFACU ili kukiwezesha kufanya kazi zake za kuwahudumia wakulima, kutokana na ukweli kwamba ni miaka mingi imepita wamekuwa wakihujumiwa na wafanyabiashara wajanja ambao ni walanguzi wa zao hilo la kahawa.
  
Sambamba na hilo anaongeza kuwa kwa kushirikiana na wakulima hao wa zao la kahawa katika kulifanya liwe endelevu pia amefanikiwa tangu aingie madarakani kuhamasisha wakulima waweze kuanzisha mashamba mapya ambayo wanatarajia kuanza kupanda aina mpya ya miche ya kahawa ambayo haishambuliwi na magonjwa kwa urahisi.

“Nikiwa Mbunge ninao wajibu wa kuhakikisha kwamba wataalamu wa kilimo wanakuwa karibu na wakulima wangu wakati wote, ili waweze kuwapatia elimu juu ya namna ya kuboresha mashamba yao ya kahawa waweze kuepukana na magonjwa ambayo yanatishia uhai wa zao hili”, anasema Msuha.
  
Akielezea juu ya masoko ya mazao hayo hususan yale ya nafaka ikiwemo mahindi yeye binafsi kwa kushirikiana na serikali, amefanikiwa kuwashawishi moja kwa moja wakulima vijijini wauze zao hilo katika vituo maalum kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali.

Pia anasisitiza kuwa ataendelea kuhamasisha wakulima wajiunge pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili waweze kuondokana na umaskini kwani kupitia vikundi hivyo wataweza kupata mikopo kwa urahisi kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.

Katika hatua nyingine akizungumzia juu ya masuala ya sekta afya anasema sera ya Wizara ya afya inasema kila kijiji kinapaswa kujenga zahanati na kituo cha afya katika kila kata hivyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ameendelea kuhamasisha wananchi watekeleze hilo, ambapo mpaka sasa kazi ya ufyatuaji tofari kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo umefanyika katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Katika sekta ya elimu anasema kuwa hivi sasa kila kata imefanikiwa kukarabati majengo ya shule za msingi na kujenga sekondari za kata na kwamba anawaomba wadau wa elimu popote walipo ndani na nje ya jimbo la Mbinga vijijini, kuhakikisha kwamba wanashirikiana kwa pamoja kujenga sekondari ya kidato cha tano na sita ili kumaliza kero hiyo ambayo inawakabili wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne.

Aidha katika hilo ameweza kushirikiana na wananchi kuendelea na kazi ya ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa na matundu ya vyoo katika baadhi ya shule huku yeye binafsi akichangia vifaa vya viwandani ikiwemo mifuko ya saruji, nondo na bati.

Vilevile kwa sekta ya miundombinu ya barabara yeye kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya na Wakala wa barabara (TANROADS) mkoani Ruvuma, amekuwa akiendelea kuwaelekeza maeneo yenye changamoto kubwa na ambayo yamekuwa hayapitiki hasa nyakati za masika ili wayafanyie matengenezo ya kudumu na hatimaye wananchi waweze kuondokana na kero hiyo.

“Kuna barabara kama vile ya njia panda kutoka Kigonsera hadi Matiri tumefanikiwa kuikarabati ambapo hivi sasa tunaendelea na mchakato ambao utalenga kufanikisha matengenezo ya barabara ya Mbinga hadi Litembo kwani hali ya barabara hii sio nzuri hata kidogo”, anasema Msuha.

Kadhalika kwa upande wa sekta ya maji na utunzaji wa mazingira, anaeleza kuwa yeye kwa kushirikiana na watendaji husika wa serikali kutoka katika idara hizo wamekuwa wakihamasisha zoezi la upandaji wa miti katika vyanzo vya maji ili visiweze kukauka.

Vilevile Msuha anasisitiza pia wananchi wamekuwa wakisisitizwa kutunza miundombinu ya maji iliyopo sasa, ambayo imejengwa na serikali ambapo pia anao mpango endelevu wa kuendelea kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.

Anabainisha kuwa Mbinga vijijini ina fursa nzuri ya kuharakisha maendeleo na uchumi kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa jimbo hilo linamazingira mazuri ambapo kama yatafanyiwa kazi ipasavyo vipato vya wananchi wake vitaongezeka.

Suala la upatikanaji wa umeme vijijini, anapongeza jitihada za serikali kupeleka nishati hiyo muhimu kwa wananchi waishio katika maeneo hayo kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambapo kwa kutekeleza hilo uchumi wa wananchi hao utasonga mbele na kwamba katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo ataendelea kuwasiliana na wakala huyo ili hatimaye aweze kupeleka huduma hiyo katika maeneo yaliyosalia.

Hata hivyo anasema katika hili anatoa wito kwa wananchi wa jimbo la Mbinga vijijini na wanachama wa Chama cha mapinduzi jimboni humo, waendelee kujenga umoja waache malumbano na wavunje makundi yasiyokuwa ya lazima badala yake waongeze juhudi katika kufanya kazi za maendeleo kwa kujenga ushirikiano ili kuweza kufikia malengo husika.


No comments: