Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa ameuagiza uongozi wa serikali ya mkoa wa Mtwara kuwakamata mara moja
viongozi wanne wa Bodi ya zao la korosho Tanzania, akiwemo Kaimu Meneja mkuu wa
Chama cha ushirika wilaya ya Masasi (MAMCU) mkoani humo Kelvin Rajab baada ya
kubaini kuwepo mapungufu makubwa ya wizi wa korosho za wakulima.
Majaliwa alitoa agizo hilo leo alipokuwa kwenye kikao cha
majumuisho ya ziara yake ya siku nne ya kikazi mkoani Ruvuma, kwenye ukumbi wa
mikutano Ikulu ndogo mjini Songea.
Vilevile alieleza kuwa wakulima kutolipwa fedha za mauzo ya
zao la korosho yaliyofanyika kwenye mnada wa tano Novemba 10 mwaka jana, bila
kuwepo maelezo kamilifu licha ya kuwa chama kikuu cha ushirika cha MAMCU kilishauza
zao hilo kwenye minada na malipo kufanyika.
Alieleza kuwa tani 2,138 za korosho katika maghala ya Mtandi
na Buco kutopelekwa mnadani kwa makusudi tangu Novemba 11 mwaka jana, taarifa
ya kuwepo au kutokuwepo korosho hizo kutokutolewa kwa mamlaka husika na
kuwasababishia hasara kubwa wananchi na serikali kukosa mapato yake.
Kadhalika aliongeza viongozi hao kushindwa kufuatilia malipo
ya zao hilo tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa kumi uliofanyika
Disemba 21 mwaka jana ambapo korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa
tani 503,297, Machinga Transport tani 104,200, Tastey tani 319,576 na Saweya
Impex tani 229,189.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa aliipongeza
bodi mpya ya korosho kwa kusimamia kikamilifu minada iliyofanyika ya zao hilo
na kuweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza na izingatie maelekezo ya serikali
kuhakikisha kwamba wanunuzi wa zao hilo wanaweka dhamana ya fedha za ununuzi wa
korosho kabla ya kuruhusiwa kununua.
Hata hivyo alisisitiza kwa kumtaka Mrajisi wa vyama vya
ushirika mkoani Mtwara kuona umuhimu wa kuzingatia maagizo yanayotolewa na
serikali ikiwa ni pamoja na kuziondoa changamoto za kuwalipa wakulima kwa bei
za mnada wa chini ili waweze kuuza kwa bei za mnada wa juu na mkulima alipwe
kwa bei ya mnada wake alipouza korosho na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment