Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akikagua mradi wa uoteshaji miti unaosimamiwa na Wakala wa misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Songea mkoani humo. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
UONGOZI wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya
Songea mkoani Ruvuma umetakiwa kuhakikisha kwamba, unasimamia vyema rasilimali
zitokanazo na misitu ili ziweze kuwanufaisha Watanzania wote badala ya
kujinufaisha watu wachache.
Aidha maofisa ardhi, maliasili na mazingira wilayani
humo wanapaswa kujitathimini upya katika utendaji wa kazi zao za kila siku
kwani kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya uwepo wa vitendo
vya rushwa katika ofisi zao wilayani hapa.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge alisema
hayo juzi mjini hapa akimtaka Ofisa misitu wilayani
Songea, Godfrey Luhimbo kumaliza kero hizo haraka kabla serikali haijachukua
hatua kali dhidi yake.
Dkt. Mahenge alisema kuwa serikali haitaki ubabaishaji katika
usimamizi wa rasilimali zake kwani inataka kuona namna gani rasilimali
hizo zinavyowanufaisha wananchi, ambapo amemtaka kuwa makini katika usimamizi
na utoaji wa vibali vya misitu hasa baada ya kupata taarifa kwamba vibali hivyo
hutolewa kinyume na taratibu za serikali kwa watendaji hao kuendekeza vitendo
vichafu vya rushwa.
“Nakupa masaa matatu kuanzia sasa nahitaji taarifa
sahihi ya namna unavyotoa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu, nimepata
taarifa wewe unatoa vibali kwa njia ya rushwa na umekuwa ukipeleka siku mbele
za kuwaandikia waombaji vibali hivyo ambavyo vipo katika mfumo sahihi unaokubalika
kisheria”, alisema Dkt. Mahenge.
Alisema kuwa mtumishi wa umma unapopewa jukumu la kiutendaji ni
lazima kutekeleza kwa misingi ya haki, usawa na sheria, kwani kinyume na hapo
serikali haitakuwa tayari kuendelea kufanya kazi na mtumishi wa aina hiyo
ambaye anailetea serikali hasara kubwa.
“Wewe ni mkuu wa idara umekuwa ukitoa vibali vya mdomo
badala ya maandishi, jambo hili linaashiria kuhusika moja kwa moja na vitendo
vya rushwa ipo siku tutakukamata na kukufikisha katika vyombo vya sheria,
taarifa niliyonayo Ofisini kwangu mchango wa idara yako kiuchumi ni mdogo wewe
unatumia ofisi ya umma kwa kujinufaisha wewe binafsi”, alisema.
Kufuatia hali hiyo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Songea,
Palolet Mgema kuhakikisha kwamba anasimamia vizuri utekelezaji wa
rasilimali za misitu katika wilaya hiyo, kwa kila alichoeleza kuwa imebainika kwamba
kuna baadhi ya watumishi wa idara hiyo ni mizigo ambapo wanafanya kazi kwa
mazoea na hawana mchango kwa taifa hili.
Sambamba na hilo amewataka kulipatia umuhimu suala la
usimamizi wa misitu na utoaji vibali halali kwa wafanyabiashara kwa sababu
wapo baadhi yao wanavuna magogo ya miti hupasua mbao na wengine kuchoma mkaa
bila kibali kilichotolewa na serikali.
Katika hatua nyingine Dkt. Mahenge ameziagiza halmashauri
zote nane zilizopo mkoani Ruvuma, kuweka alama zinazoonesha mipaka na maeneo ambayo
hayaruhusiwi kufanyika shughuli za kibinadamu kama vile kilimo ili kuweza kulinda
vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira.
Vilevile kwa upande wake Meneja wa Wakala wa huduma za misitu
wilaya ya Songea, Manyise Mpokigwa ameiomba serikali kuona umuhimu wa kusaidia
katika suala zima la ulinzi wa misitu hiyo kwani kasi ya uchomaji moto na mkaa imekuwa
kubwa jambo ambalo linaharibu uhai wa misitu hiyo ikiwemo uoto wake wa asili.
Mpokigwa alisema bado TFS inaendelea na kazi ya upandaji
miti katika maeneo mbalimbali kama vile Wino, Mahanje pamoja na kugawa mbegu za
miti kwa wananchi ambao wanaendelea kupanda katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment