Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
BAADHI ya Wananchi wanaoishi katika wilaya ya Nyasa mkoani
Ruvuma wamelalamikia ujenzi wa barabara ya kutoka Mbinga mjini hadi Mbamba bay
wilayani humo, iliyopo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa
kutofuatilia kwa karibu ujenzi unaoendelea sasa, hali ambayo inasababisha
barabara hiyo kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara.
Aidha walisema kuwa wanashangaa kuona ikifanyiwa matengenezo
kwa mara ya pili na mkandarasi mwingine, wakati ni miezi michache tu imepita
kulikuwa na mkandarasi ambaye alikuwa akiitengeneza.
Wameiomba serikali kupitia Wakala huyo wa TANROADS kuwabana
wakandarasi wazembe wanaopewa kazi ya kujenga barabara wilayani hapa, ili
kuepuka barabara hizo kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara jambo ambalo
linaisababishia serikali hasara kubwa juu ya upotevu wa fedha za wananchi.
Pia walifafanua kuwa hata baadhi ya barabara zinazojengwa
katika maeneo mbalimbali wilayani Nyasa ambazo zinasimamiwa na Wakala huyo,
hazina ubora licha ya kutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kuelekezwa katika
miradi mingine ya maendeleo.
Hivi sasa wameutaka uongozi wa TANROADS mkoa wa Ruvuma
kumfuatilia mkandarasi anayefanya ukarabati wa barabara inayoanzia Mbinga
mjini kwenda kijiji cha Burma, kupitia kona hatari za
Ambrosi hadi daraja la mto Ruhekei kuhakikisha
kwamba anasambaza kifusi anachomwaga barabarani kwa wakati na kiwango
kinachotakiwa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa watumiaji wengine wa
bara bara hiyo.
Simbert Ndunguru alieleza kuwa vifusi vinavyomwaga
vinachelewa kusambazwa jambo ambalo linawafanya madereva wa magari hasa ya
abiria kupita kwa taabu na wakati mwingine, hulazimika kupita upande ambao una
bonde kubwa lenye kuhatarisha usalama wa magari hayo na abiria waliopanda kwa
lengo la kukwepa vifusi vinavyomwagwa barabarani humo.
“Barabara hii ya Mbinga mjini hadi kwenda Nyasa ina kona
nyingi ambazo ni hatari, huyu mkandarasi anapaswa kila anapomwaga kifusi
akisambaze kwa wakati na sio kukiacha kwa muda mrefu bila kusambaza, kwani
kumekuwa na usumbufu mkubwa wakati wa kupita na magari yetu”, alisema.
Naye Ally Komba aliongeza kuwa endapo mkandarsi huyo
atachelewa kusambaza kifusi hicho katika barabara hiyo, ipo siku kuna hatari ya
kutokea ajali hasa nyakati hizi za masika pale mvua zitakapoendelea kunyesha.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania mkoani Ruvuma, Razak
Alinanuswe alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo
hakuweza kupatikana na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila
kupokelewa.
No comments:
Post a Comment