Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
TIMU ya viongozi wa serikali mkoa wa Ruvuma imewasili
wilaya ya Nyasa mkoani humo kwa lengo la kushiriki tamasha la uzinduzi wa fursa za
utalii huku serikali ikiwataka wadau kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje
ya mkoa huo kuwekeza wilayani humo kwenye shughuli za uvuvi, ujenzi wa hoteli
za kisasa pamoja na viwanda vidogo vidogo.
Aidha imeelezwa kuwa ujenzi wa viwanda hivyo utasaidia
kuifanya wilaya hiyo ipige haraka hatua mbele za kimaendeleo katika kuongeza
thamani ya mazao yanayozalishwa, kukuza uchumi na kuleta ajira kwa vijana.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema hayo
juzi alipokuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la uzinduzi wa fursa za utalii na
kuinua uchumi wilayani Nyasa lililofanyika katika kituo cha udhibiti wa
rasilimali za uvuvi wilayani humo.
Vilevile tamasha hilo lilishirikisha viongozi hao wa ngazi
mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za utalii zilizopo wilayani humo,
ikiwemo fukwe za ziwa Nyasa samaki wa mapambo wenye rangi za aina mbalimbali, mazoezi
ya kuogelea, visiwa vilivyopo ndani ya ziwa hilo, milima, mawe yenye kuvutia,
shughuli za uvuvi na historia ya mambo ya kale.
Dkt. Mahenge aliwapongeza viongozi wa wilaya hiyo kwa kazi
wanazozifanya katika kupigania maendeleo ya wananchi ambapo alisisitiza kwa
kuwataka jitihada hizo ziendelezwe kwa kuwa wabunifu zaidi na kwamba serikali
itaendelea kuunga mkono kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017
kuelekea 2018 serikali kuanzia mwezi Februari mwaka huu, itaanza kujenga
barabara ya kutoka Mbinga mjini hadi Mbamba bay wilayani Nyasa kwa kiwango cha
lami.
“Sisi kama serikali tutahakikisha tunafungua fursa hizi
muhimu kwa kujenga barabara zilizokuwa katika viwango bora na tayari
tumetangaza kujenga barabara hii kwa kiwango bora cha lami hivyo ili utalii
uweze kutuletea mapato katika wilaya yetu ni lazima tuanze sasa kuwekeza kwanza
sisi wenyewe”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
Pia aliongeza kuwa fursa zinapokuja wananchi wanapaswa
kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa wepesi kushiriki shughuli mbalimbali za
kimaendeleo kama vile kilimo cha mazao ya chakula na biashara ambayo yataweza
kuwaletea kipato.
Hata hivyo tamasha hilo la uzinduzi wa fursa za utalii
wilayani Nyasa ni endelevu na kwamba litakuwa likiadhimishwa kila mwaka ifikapo
Disemba 30 kwa lengo la kutangaza na kukuza fursa za kiuchumi wilayani hapa,
ikiwemo masuala ya utalii wa ndani ambao wananyasa wenyewe wanalojukumu kubwa
la kuuimarisha ili uweze kuwa endelevu na kuwaletea kipato kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kijacho.
No comments:
Post a Comment