Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inakabiliwa
na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za
sekondari jambo ambalo linarudisha nyuma, maendeleo ya mkoa huo kwa watoto
wanaopenda kusoma masomo hayo.
Aidha imeelezwa kuwa mahitaji ya walimu wa masomo ya sayansi
katika Manispaa hiyo ni walimu 375 ambapo waliopo sasa ni 132 tu, hivyo kuwa na
upungufu wa walimu 243.
Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo amewaeleza
waandishi wa habari kuwa Manispaa ina ziada ya walimu 192 wa masomo ya sanaa,
katika shule za sekondari ambapo mahitaji ya walimu katika masomo hayo ni 536
wakati walimu waliopo ni 728.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa katika shule za sekondari 24
za serikali zilizopo katika Manispaa ya Songea zina jumla ya walimu 856
wanaofundisha masomo ya sayansi na sanaa.
Kwa mujibu wa Ofisa habari huyo anafafanua kwamba pia katika
shule za msingi 76 za serikali zenye jumla ya wanafunzi 50,119 wakiwemo
wavulana 24,656 na wasichana 25,463 zina upungufu wa walimu 95 wa masomo
mbalimbali.
Hata hivyo aliitaja mikakati ya kukabiliana na changamoto
hizo, kuwa Manispaa hiyo imeomba Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kutoa
kipaumbele kwa mikoa ya pembezoni kuwapangia idadi kubwa ya walimu wa sayansi
badala ya kupangiwa walimu wa masomo ya historia, kiswahili na jiografia ili
kuweza kuziba pengo hilo.
No comments:
Post a Comment