Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAKALA wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea
mkoani Ruvuma, ametakiwa kuhakikisha kwamba mahindi yote yaliyonunuliwa yanatunzwa
vizuri kwa umakini mkubwa, hayaharibiki katika maghala ya kuhifadhia chakula
ili yaweze kusaidia pale itakapotokea tatizo la njaa hapa nchini.
Agizo hilo limetolewa jana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa ametembelea kituo cha hifadhi
hiyo kilichopo katika Manispaa ya Songea mjini hapa.
“Hakikisheni mahindi haya yanatunzwa vizuri ili yasiweze
kuharibika, yasije yakatokea kama msimu uliopita mwaka jana mahindi mengi
yaliharibika hivyo serikali hatutaki kuona tena mwaka huu tatizo hili
linajirudia”, alisisitiza Majaliwa.
Alifafanua kuwa serikali kupitia kitengo chake cha kuhifadhi
chakula kila mwaka kipo kwa ajili ya kununua kiasi kidogo cha ziada ya chakula
na sio vinginevyo, ikiwa ni lengo la kuweka tahadhari pale yanapotokea matatizo
ya njaa.
“Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi mwaka hadi mwaka, kwa
ajili ya kununua chakula hivyo ni wajibu wa wafanya kazi wa idara hii kukitunza
ili kisiweze kuharibika kwa ajili ya matumizi ya baadaye”, alisema.
Kadhalika alieleza kuwa endapo kuna kiongozi yeyote wa
serikali ana wasiwasi juu ya hali iliyopo katika msimu wa mwaka huu, kutokana
na mvua kuchelewa kunyesha na hali ya joto kali tofauti na misimu mingine ni
muhimu kuwahimiza wananchi wajiwekee akiba ya chakula ili kiweze kuwasaidia
katika familia zao.
NFRA Kanda ya Songea imepongezwa pia kwa juhudi kubwa inazofanya ya
ununuaji wa mahindi, pamoja na kwamba haikutimiza lengo la serikali kutokana na
ushindani mkubwa wa kibiashara kutoka kwa watu binafsi.
Awali Meneja wa Wakala huyo wa hifadhi chakula Kanda ya
Songea, Majuto Chabuluma alimweleza Waziri Mkuu kwamba, serikali katika
bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 iliidhinisha kwa wakala wa taifa wa
hifadhi ya chakula kununua jumla ya tani 100,000 za mahindi kwa nchi
nzima.
Kwa kanda ya Songea mkoani Ruvuma ilipangiwa kununua tani
22,000 kutoka kwa wakulima katika maeneo ya vijijini ambapo kazi ya ununuzi huo
ilianza Aprili 22 mwaka jana baada ya kukamilisha ufunguzi wa vituo 26 vya
ununuzi wa mahindi.
Majuto alieleza kuwa vituo hivyo vilifunguliwa katika maeneo
ya vijijini kwa lengo la kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha kwamba,
wakala anawafikia wakulima wa mahindi kwa bei nzuri inayotolewa na serikali.
Hadi kufikia Disemba 27 mwaka jana Kanda ya Songea ilikuwa
imekwisha nunua tani 10,335,256 za mahindi kati ya tani 22,000 ambazo
zilipangwa kununuliwa na kwamba changamoto kubwa iliyojitokeza kwenye zoezi la
ununuzi wa msimu huo ni mwenendo usioridhisha wa wakulima katika kupeleka mazao
yao kwenye vituo vya ununuzi vya NFRA ambapo mengi walikuwa wakiyauza kwa
wafanyabiashara binafsi hivyo kufanya wakala huyo kushindwa kufikia malengo
husika.
Aidha Majuto alisema kuwa sababu nyingine iliyochangia hilo
ni kuchelewa kuanza kwa zoezi la ununuzi ambapo kawaida msimu wa ununuzi hufunguliwa
baada ya mwaka wa fedha wa serikali, yaani mwezi Julai ambapo hazina hutuma
fedha kwa wakala kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo baada ya vikao vyao vya
bajeti kumaliza kuketi.
Katika msimu wa mwaka huu maeneo mengi mkoani Ruvuma
yanakabiliwa na upungufu wa chakula hivyo wanunuzi wengi binafsi waliwahi
kwenda huko kwa wakulima, kununua mahindi na kuyahifadhi katika maghala yao
ikizingatiwa kwamba mkoa huo ni tegemeo kubwa la kutoa chakula cha ziada kwa
maeneo mengine hapa nchini.
Hata hivyo sababu nyingine iliyojitokeza ya
kushindwa kufikia malengo alisema kuwa ni pamoja na ushindani wa bei ambapo
bei iliyotolewa na wanunuzi binafsi ilikuwa juu tofauti na ile iliyotolewa na
serikalia kwa NFRA.
No comments:
Post a Comment