Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAFANYABIASHARA
katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kuweka
utaratibu kwa makampuni mawili yanayojishughulisha na uchimbaji madini mkoani
hapa, kulipia kodi mkoani humo badala ya Dar es salaam ili yaweze kusaidia
kupunguza makali ya shilingi bilioni 12 ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
mkoani Ruvuma imepangiwa kukusanya mwaka huu toka kwa wafanyabiashara hao.
Ombi hilo
lilitolewa jana na wafanyabiashara hao kwenye mkutano uliofanyika baina yao na
uongozi wa TRA makao makuu jiji Dar es Salaam, uliofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Songea Club uliopo mjini hapa.
Akichangia hoja
kwenye mkutano huo mmoja wa wafanyabiashara hao Jaribu Mangoma alisema kuwa
kutokana na kitendo cha serikali kuyaachia makampuni ya TANCOAL Eenergy
inayojishughulisha na uchimbaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji
cha Ntunduaro wilayani Mbinga na kampuni ya MANTRA inayofanya utafiti wa
upatikanaji wa madini aina ya Urani, eneo la mto Mkuju wilayani Namtumbo ndiyo
yanayochangia wafanyabiashara kukadiriwa kodi kubwa ambayo inawafanya baadhi yao
wafilisike na wengine kufunga maduka yao.
Mfanyabiashara
mwingine Omary Chika amelalamikia kuwepo kwa mrundikano wa kodi ambao umeonekana
kuwa ni kero hivyo ameshauri Mamlaka ya mapato Tanzania, kuona umuhimu wa kuwa
na tozo moja kwa kila mfanyabiashara ambayo itaunganisha kodi zote zinazotolewa
hivi sasa kwa lengo la kupunguza kero na usumbufu wanaoupata wafanyabiashara
hao.
Naye Emmanuel
Kondowe pia ameishauri kufanyia marekebisho sheria ya kuwatoza wafanyabiashara
wa nyumba za kulala wageni na hoteli kwa kulipa kodi kwa vigezo vya dola badala
ya fedha ya kitanzania, jambo ambalo limekuwa likileta mgogoro baina ya
wafanyabiashara hao na TRA ambayo imekuwa ikiwalazimisha walipe kwa mfumo wa dola
wakati baadhi ya wateja wao hawana uelewa wa matumizi ya dola.
Kwa upande wake Katibu
mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Ruvuma Wilson Nziku alisema
kuwa jamii ya wafanyabiashara hapa nchini, bado haina uelewa wa kutumia mashine
za Kielektroniki (EFD) hivyo ameiomba serikali kutoa muda maalumu kwa TRA kutoa
elimu ya kutosha huku akihoji pia kwa nini wafanyabiashara hao wameambiwa
wanunue mashine hizo wakati serikali ilikwisha tangaza kwamba inatoa bure.
Kwa upande wake
Naibu Kamishna mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania, Charles Kichele amewataka
wafanyabiashara hapa nchini kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati kwani
kufanya hivyo ni kuijenga nchi yao kwa maendeleo sasa na vizazi vijavyo.
“Mkilipa kodi kwa
wakati serikali itaweza kutengeneza miundo mbinu ya barabara, hospitali na
taasisi mbalimbali za elimu ikiwemo vyuo vikuu nashauri pia wafanyabiashara
tunzeni kumbukumbu zenu za biashara mnazofanya kwa kutumia mashine za EFD
ambazo zitawasaidia kupunguza kero zinazojitokeza wakati wa kukadiriwa kodi”,
alisema Kichele.
Kichele aliwapongeza
wafanyabiashara wa mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano mkubwa wanaouonyesha baina
yao na TRA kwa madai kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wa maeneo mengine
wamekuwa wakitoa michango ya kubomoa na sio kujenga huku akiongeza kuwa Mamlaka
hiyo itahakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
wanafanyabiashara hao mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment