Na Mwandishi wetu,
Songea.
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani
Ruvuma, limewatahadharisha Wananchi wa mkoa huo hususan kwa wale wanaoishi
vijijini kuwa makini na watu wanaotumia jina la shirika hilo, kuwatapeli fedha
kwa kisingizio cha kuwaingizia umeme majumbani mwao kupitia Mpango wa Umeme Vijijini
(REA) katika awamu hii ya tatu.
Aidha limewataka kuwa na mazoea ya kutoa taarifa kwa shirika
hilo pale wanapoona kuna watu wanaokwenda kwenye maeneo yao, kwa
kujifanya maofisa wa TANESCO na kuanza kuchangisha fedha kwa kuwa
wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni shirika hilo na sio vinginevyo.
Hatua hiyo inafuatia tukio la hivi karibuni la maofisa wa shirika
hilo kikosi cha usalama kwa kushirikiana na wananchi kuwatia mbaroni vijana wanne
wa Kampuni ya Syba Electrical Service and General Enterprises inayofanya kazi
ya ukandarasi wa umeme, yenye makao makuu yake mkoani Mwanza baada ya vijana
hao kujitambulisha kama maofisa wa TANESCO wakiwa tayari wamekusanya zaidi ya
shilingi 700,000 kutoka kwa wakazi wa kijiji cha Mbinga Mhalule wilayani Songea
mkoani hapa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja wa shirika
la TANESCO mkoa wa Ruvuma, Mhandisi John Kiduko ni kwamba tukio hilo
lilitokea Disemba 24 mwaka jana majira ya saa nne asubuhi ambapo
vijana hao walikamatwa na maofisa wa shirika hilo, kitengo cha usalama kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa kutoka
kwa raia wema.
Kiduko alifafanua kuwa watu hao walikamatwa baada ya kutiliwa
mashaka na uwepo wao kijijini hapo, kwani walianza kukusanya fedha kwa kaya
17 sawa na shilingi 140,000 ambapo kwa kila kaya ilitoa shilingi 20,000 ikiwa
ni gharama ya kuunganishiwa umeme kupitia Mpango wa Umeme Vijijini (REA).
Aidha Kiduko alifafanua kuwa siku hiyo ya Disemba 24 mwaka
jana vijana hao walirudi tena na kuanza kupita kwa kaya moja hadi
nyingine ambapo walifanikiwa kukusanya shilingi 600,000 kutoka kaya 30, hata
hivyo baadhi ya wananchi hao waliwatilia mashaka vijana hao na
kuanza kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kijiji ambaye alipopiga simu TANESCO,
waliwajulisha Polisi juu ya tukio hilo na hatimaye waliwakuta vijana hao na
kuwaweka chini ya ulinzi wa wananchi ambapo walipohojiwa walisema wanatoka Kampuni
ya Syba Electrical Service and General Enterprises na kuweza
kufanikiwa kuwakamata.
Kwa mujibu wa Kiduko alisema kwamba kwa kawaida hakuna mtu
ambaye amepewa ruhusu ya kukusanya fedha ikiwa ni gharama za wananchi
kuunganishiwa umeme, badala yake gharama hizo zinatakiwa kulipwa kwa shirika
hilo tena watu kufika ofisini na kupatiwa risiti halali, hivyo amewatahadharisha
wananchi kuwa makini na matapeli na watu wenye nia ya kulichafua shirika la
umeme Tanzania.
Aliongeza kuwa siku moja kabla ya kukamatwa kwa watu hao
yaani Disemba 23 mwaka jana tayari walifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi
140,000 kwa kaya saba na siku ya pili ndipo walirudi tena kuendelea na wizi huo
kwa kuwakatia wananchi risiti feki ambapo walifanikiwa kukusanya shilingi 600,000
kutoka kaya 30.
Kiduko ametoa wito kwa vyombo vya habari vilivyopo mkoani
Ruvuma, kusaidia kuujulisha umma wa Watanzania juu ya kuwepo kwa matapeli wa
aina hiyo ambao wameanza kupita vijijini na kuwadhulumu wananchi fedha zao wakitumia
jina la Tanesco.
Vilevile alisema kuwa kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa
mpango wa REA awamu ya tatu,Tanesco itafanya mikutano katika vijiji vyote
vitavyoingizwa katika mpango huo na itafungua ofisi ndogo katika kila kijiji
na kuwajulisha wananchi kuhusiana na utaratibu wake ambapo zaidi ya
vijiji 437 katika mkoa wa Ruvuma, vitapata umeme kupitia mpango huo.
Akijibu tuhuma hizo Mkurugenzi wa Kampuni ya Syba Electrical
Service and General Enterprises, Silvester Jumanne alikana kuwepo kwa tukio
hilo na kusema kwamba hakuna mfanyakazi wake aliyekamatwa kuhusiana na tukio
hilo kwani kazi waliyopewa na Tanesco ni kufanya wayaringi majumbani na sio kuingiza
umeme majumbani.
Alisisitiza kuwa hao ni watu matapeli wanaotaka kuchafua jina
la shirika hilo na amewataka TANESCO kuongeza nguvu katika kuwasaka watu
wanaofanya utapeli wa aina hiyo kwa wananchi.
“Nashauri hao vishoka wanaojifanya ni Kampuni ya Syba wapelekwe
tu mahakamani mimi siwafahamu kabisa na mimi sijawahi kufika huko na sipafahamu
Mbinga Mhalule”, alisema Jumanne.
No comments:
Post a Comment