Sunday, January 22, 2017

MANISPAA SONGEA YAPITISHA BAJETI SHILINGI BILIONI 63 KWA AJILI YA MAENDELEO YA WANANCHI

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma limepokea, kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2017/2018 zaidi ya shilingi bilioni 63.7 kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ya wananchi katika halmashauri hiyo.

Akiwasilisha bajeti hiyo Mchumi Mkuu wa Manispaa hiyo, Raphael Kimary alibainisha kuwa kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 16 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo ni ruzuku kutoka serikali kuu na shilingi bilioni 1.785 ni fedha pia za utekelezaji maendeleo ya wananchi.
Mchumi Mkuu wa Manispaa ya Songea, Raphael Kimary akiwasilisha bajeti.

Kwa mujibu wa Kimary alieleza kuwa fedha za matumizi ya kawaida ambazo ni ruzuku kutoka serikali kuu zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni 3.893 na matumizi ya kawaida kutoka vyanzo vya ndani zimetengwa shilingi bilioni 1.533.

Alisema kuwa mishahara ya watumishi wametenga shilingi bilioni 40 na nguvu za wananchi zimetengwa shilingi milioni 175.


Vilevile ameliambia baraza la Madiwani wa Manispaa ya Songea kwamba uandaaji wa mpango wa bajeti hiyo umezingatia miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na serikali ikiwemo ukusanyaji wa mapato na utengaji rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa kwa miaka mitano ijayo kuanzia 2017 hadi 2021.

Alibainisha kuwa bajeti hiyo imejikita zaidi katika sekta kipaumbele nane ambazo zimepatiwa mafunzo ya utekelezaji ambazo zilizopo katika Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, wazee na watoto, Wizara ya maji na umwagiliaji na Wizara ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi.

Sekta nyingine zilizopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni kutoka Wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi, Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia, Wizara ya fedha na mipango, Wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji na Wizara ya nishati na madini.


Kadhalika amesisitiza kuwa bajeti hiyo pia imezingatia hotuba ya Rais Dkt. John Magufuli aliyoitoa katika Bunge la 11, hotuba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya Januari mwaka huu katika mkoa wa Ruvuma, ambayo ilikuwa na masuala mtambuka na maelekezo ya viongozi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

No comments: