Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa ameitaka kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya makaa ya
mawe Tancoal Energy, kwenye mgodi wa Ngaka wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma,
kutekeleza makubaliano ambayo yapo kwenye mikataba kabla serikali haijachukua
hatua zaidi.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu Majaliwa jana alipokuwa
akizungumza na viongozi mbalimbali wa mkoa huo kwenye kikao cha majumuisho ya
ziara yake ya siku nne ya kikazi mkoani hapa, ya kutembelea na kukagua miradi
ya maendeleo ambapo alisisitiza kuwa endapo kampuni hiyo haitatekeleza
makubaliano husika ya mikataba iliyoingia na serikali, italazimika kuizuia
isiendelee na kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kuitafuta kampuni nyingine
ambayo itaridhia makubaliano ambayo yataleta manufaa kwa Watanzania juu ya
uendeshaji wa mgodi huo.
Pia alieleza kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanyika kwenye
mgodi huo, amebaini kuwepo kwa mapungufu mengi yakiwemo Shirika hilo la
maendeleo la taifa kutolipwa gawio lake (Dividend) tangu ulipoanza uzalishaji
wa makaa hayo mwaka 2011.
Waziri Mkuu huyo alifafanua kuwa kampuni hiyo pia imeanza
kuzalisha na uzalishaji huo unaendelea kuongezeka siku hadi siku, pia serikali
imefanikiwa kuongeza masoko kwa kuzuia uingizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ya
nchi ambapo Tancoal Energy ya Ngaka wilayani Mbinga na Tanzacoal ya Kiwira
wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, zinazotokana na kampuni moja ya Australia Intra
Energy Corporation Limited (IEC) ndio wazalishaji wakubwa wa makaa hayo hapa
nchini lakini kampuni ya Tancoal inaeleza kwamba inapata hasara kila mwaka
jambo ambalo amedai kuwa sio la kweli.
“Kampuni inatuambia kila mwaka imekuwa inapata hasara jambo
hili haliaminiki, serikali haitakubali kuona hali hii inaendelea nataka
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akague mahesabu yote ya
kampuni hii ikibainika wanadanganya, Tancoal Energy watawajibika kulipa gawio
la serikali tokea mgodi ulipoanza”, alisisitiza.
Vilevile amemtaka Mwanasheria mkuu wa serikali aone umuhimu
wa kupitia upya mkataba baina ya kampuni hiyo ya mgodi wa makaa ya mawe na Shirika
la maendeleo la taifa, ili kuuboresha na pia kuona uwezekano wa kuongeza hisa
za NDC pia kama itashindikana washauri namna ya Tancoal Energy kujitoa katika
mkataba huo.
Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka pia Wizara ya viwanda na
biashara isimamie kikamilifu utendaji wa NDC pamoja na kampuni ya Tancoal
Energy ili kuhakikisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkataba huo,
yanatekelezwa ipasavyo na kwamba serikali ishauriwe namna ambavyo mapungufu
yote yatakavyoondolewa.
Hata hivyo Waziri Mkuu huyo ameishushia lawama kampuni hiyo
kuwa hadi sasa haijatekeleza makubaliano yaliyofikiwa na serikali katika
mikataba husika ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kutoka kijiji
cha Kitai ambako kuna bandari kavu ya kupakia makaa ya mawe hadi mgodini
yanakochimbwa makaa hayo, ujenzi wa mitambo ya ufuaji wa umeme na kuimarisha
tekinolojia ya kuchimba makaa hayo ya mawe.
No comments:
Post a Comment