Na Kassian
Nyandindi,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,
Luckness Amlima ametishiwa kifo kwa maneno na mwananchi mmoja wa wilaya hiyo
Gerold Haulle wakati alipokuwa akitekeleza zoezi la kuwahamisha wananchi
wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye chanzo cha maji, ambacho ni tegemeo
kubwa kwa hifadhi ya maji kwa wakazi wa mji wa Namtumbo.
Ofisa habari wa wilaya hiyo Yeremias
Ngerangera alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 19 mwaka huu majira ya
mchana wakati Mkuu huyo wa wilaya alipokuwa ofisini kwake na mwananchi huyo,
akimhoji na kumtaka asitishe shughuli zake za kilimo ambazo amekuwa akizifanya
kwenye chanzo kikuu cha maji ya mto Rwinga uliopo wilayani humo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Amlima amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo la kutishiwa kuuawa kwa maneno huku akiongeza kuwa
taarifa zimefikishwa kituo kikuu cha Polisi wilayani Namtumbo kwa hatua zaidi.
“Tunamtaka mwananchi huyu aondoke
kwenye chanzo hiki cha maji kwa sababu ni tegemeo kubwa kwa wananchi wengi wa
mji wa Namtumbo, endapo akiendelea kufanya shughuli zake za kilimo ambazo
zinaharibu mazingira ya chanzo hiki ni hatari kwa wananchi wangu kukosa huduma
ya maji”, alisema Amlima.
Aliongeza kuwa licha ya kupewa
kitisho hicho cha kifo ametoa wiki moja kwa kumtaka mwananchi huyo aondoke
katika eneo hilo la chanzo na kuacha shughuli zake za kibinadamu, kwa kuwa
suala hilo ni la kisheria na endapo ataendelea kukaidi atafikishwa mahakamani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma,
Zubery Mwombeji alipoulizwa na mwandishi wetu alisema kuwa tukio hilo bado
halijamfikia ofisini kwake na kwamba anafanya ufuatiliaji wa kina na kwamba
atalitolea taarifa baadaye.
No comments:
Post a Comment