Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na wananchi katika mikutano yake mbalimbali ya kusisitiza maendeleo mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amewapiga marufuku
viongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani humo kuendelea kuwachangisha fedha wananchi
wa wilaya hiyo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya vya maabara na majengo
mengine ya madarasa, hadi pale watakapokamilisha kuweka vifaa vinavyohitajika kwa
majengo yaliyokuwa tayari.
DKt. Mahenge amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada
ya kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wakazi wa Mbinga mjini, wakieleza
kuwa wamekamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara lakini bado havijaanza kutumika
kwa kuwa serikali kupitia halmashauri ya mji huo haijapeleka vifaa hivyo kwa
ajili ya matumizi ya wanafunzi.
Wakazi hao wa mji wa Mbinga walimuomba Dkt. Mahenge
kutoa ufafanuzi juu ya michango hiyo inayoendelea kuchangishwa na Watendaji wa mitaa
na kata, ambao wanawalazimisha wananchi kuendelea kutoa fedha licha ya
kukamilika kwa vyumba vya maabara katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa sio busara
kwa Watendaji hao kuendelea kuchangisha fedha wananchim, kwani kila
shule ya sekondari ya serikali kuna maabara na sasa kilichobaki ni
halmashauri kuhakikisha zinapeleka vifaa husika ili maabara hizo
ziweze kuanza kutumika.
Alisema kuwa agizo hilo pia linahusu hata katika miradi
mingine kama vile zahanati, vituo vya afya na hata katika maeneo
mengine ambako wananchi wameonekana kutekeleza wajibu wao na upande uliobaki
ni wa serikali kupeleka vifaa, madaktari na dawa.
“Viongozi wenzangu lazima tuwe wa kweli, hakuna sababu
ya kuendelea kuwataka wananchi wachangie fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara
wakati zilizopo bado hazijaanza kutumika sasa nawashauri Wakurugenzi wa
halmashauri za wilaya katika mkoa wetu Ruvuma, kuhakikisha mnapeleka vifaa husika
ili maabara hizi zianze kutumika”, alisema Dkt. Mahenge.
Alisema kuwa lengo la serikali kujenga maabara hizo ni
kuwajengea uwezo watoto waliopo shuleni waweze kusoma masomo ya sayansi, huku
akisisitiza kuwa hakuna ulazima wa kuanza ujenzi mwingine wa majengo hayo hadi
pale halmashauri hizo zitakapokamilisha zoezi la upelekaji vifaa.
Alifafanua kuwa endapo itaonekana kuna maeneo ambayo bado
kazi ya ujenzi huo haijakamilika ndipo wananchi wanapaswa kushirikishwa kutoa
michango yao badala ya kuwachosha kwa kuwachangisha michango mingi isiyokuwa ya
lazima.
Pia alibainisha kuwa kwa kutambua umuhimu wa wataalamu
wa masomo ya sayansi serikali itaendelea kutenga fedha mwaka hadi mwaka, ili
kujenga na kuboresha miundombinu ya shule, afya, maji na bara bara hatua ambayo
itasaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi katika mkoa huo.
Alisema kuwa lengo ni kutaka kuona elimu inayotolewa inaendana na mahitaji halisi katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia, unaohitaji wataalamu wenye maarifa na uelewa wa kutosha katika fani mbalimbali pamoja na watu wenye afya njema na miundombinu bora.
Alisema kuwa lengo ni kutaka kuona elimu inayotolewa inaendana na mahitaji halisi katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia, unaohitaji wataalamu wenye maarifa na uelewa wa kutosha katika fani mbalimbali pamoja na watu wenye afya njema na miundombinu bora.
No comments:
Post a Comment