Na Mwandishi wetu,
Songea.
BAADHI ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma wameuomba uongozi wa Manispaa hiyo kumuhimiza Mkandarasi wa kampuni ya
Lukoro Construction Limited, ambayo imepewa kazi ya ujenzi wa barabara kwa
kiwango cha lami mjini hapa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa wakazi wa
maeneo ya Matarawe, Bombambili, Mateka na Matogoro walisema kuwa licha ya kuwa
kazi hiyo inayofanywa na mkandarasi huyo inaendelea kufanyika, lakini bado
jitihada zinahitajika kuona namna ya kumaliza ujenzi huo mapema wakidai kuwa
mvua zitakapoanza kunyesha kwa wingi zinaweza kusababisha kuchelewa kukamilisha
ujenzi huo.
Amina Komba mkazi wa eneo la Matarawe alisema kuwa Kampuni ya
ukandarasi ya Lukoro kwa muda mrefu ilianza kutengeneza barabara ya kutoka Bombambili
hadi Mwembechai, lakini mpaka sasa bado haijakamilika licha ya kuwa kuna baadhi
ya maeneo ya barabara hiyo imeanza kuharibika.
John kapinga mkazi wa eneo la Mateka naye alisema kuwa licha
ya Kampuni hiyo kuanza kujenga barabara ya kutoka shule ya sekondari ya
wasichana ya Songea hadi Matogoro haijakamilika nayo ujenzi wake kwa kiwango
hicho cha lami.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Lukoro Construction Company
Limited Mhandisi Harod Konga alipohojiwa alisema kuwa kampuni yake imekwisha anza
kufanya matengenezo ya barabara hizo zenye urefu wa kilomita 8.6 ambazo zipo katika
maeneo hayo tofauti.
Alisema kuwa ujenzi huo wa barabara kwa kiwango cha lami kwa
sasa bado haujakamilika licha ya kazi ya ujenzi huo bado inaendelea hivyo amewataka
wakazi wa Manispaa ya Songea kuondoa hofu na kuvuta subira wakati ujenzi huo
ukiwa unaendelea na kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Alizitaja barabara hizo zenye urefu wa kilomita 8.6 ni za
kutoka Matogoro hadi FBC, shule ya wasichana ya Songea hadi Mateka, Mwembechai
hadi Bombambili, eneo la Kituo kikuu cha Polisi hadi kituo cha daladala cha Mlyayoyo,
Yapenda hadi eneo la Mitumbani na kwamba mradi huo wa ujenzi ulianza Julai
mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea,
Tina Sekambo alipohojiwa na mwandishi wetu ofisini kwake kuhusiana na ujenzi wa
barabra hizo alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusiana na mkandarasi
huyo kwamba anachelewesha kukamilisha ujenzi wa barabara hizo, lakini ofisi
yake bado inafahamu kuwa mkataba unaonyesha kuwa Kampuni hiyo ya Lukoro
inatakiwa kukabidhi barabra hizo ujenzi wake ukiwa umekamilika ifikapo Juni 30
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment