Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na wananchi katika mikutano yake mbalimbali ya kuhamasisha maendeleo mkoani humo. |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amewataka
wananchi waishio katika wilaya ya Nyasa mkoani humo kufanya kazi kwa bidii ili waweze
kujiletea maendeleo yao, hatua ambayo itawasaidia kukuza uchumi katika familia
zao na wilaya hiyo kwa ujumla.
Dkt. Mahenge alisema kuwa tabia ya uvivu na kutopenda kufanya
kazi imepitwa na wakati na kwamba, ndiyo chanzo kikuu cha kuukaribisha umaskini
kwa familia zao hivyo katika kukabiliana na hali hiyo hawana budi kila mmoja
wao kutambua majukumu yao kwa kufanya kazi kwa malengo.
“Ni lazima tujenge tabia ya kujitegemea kufanya kazi kwa
bidii, hatua ambayo itasaidia kuinua pato la mtu mmoja mmoja, wilaya, mkoa na
taifa letu kwa ujumla hatutaki kuona vijana wetu wanatumia muda mwingi kucheza
michezo ya Pool kwa serikali hii huu sio muda wake”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
Hata hivyo alisema kuwa Tanzania ni nchi ambayo imekuwa ikisifika
na mataifa mengine ya nje kutokana na kukua haraka uchumi wake na nguvu kubwa
katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
No comments:
Post a Comment