Friday, January 20, 2017

TANESCO MBINGA KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA YA UMEME KWA WANANCHI WAKE

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Kanuti Punguti ambaye ni Meneja wa kituo cha kufua umeme wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, alipotembelea hivi karibuni akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika wilaya hiyo.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, inaendelea na mikakati yake ya kufikisha huduma ya nishati ya umeme kwa wananchi wa mjini na vijijini wilayani humo, ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo ili waweze kuwa na maendeleo.

Aidha serikali kupitia mpango wake wa usambazaji umeme vijijini (REA) awamu ya tatu, shirika hilo linatarajia kuwafikia wananchi wa vijiji 146 vilivyopo wilayani hapa na kwamba wametakiwa kuacha kuzuia maeneo yao kupitisha nguzo za umeme kwa malengo ya kudai fidia, wakati miradi hiyo haina fidia ya aina yoyote ile.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TANESCO tawi la Mbinga, Kanuti Punguti wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alieleza kuwa hadi sasa shirika hilo limewafikia wateja 5,612 wanaopata huduma ya umeme wilayani humo.


Punguti alifafanua kuwa kwa upande wa Mbinga mjini kuna jumla ya wateja 4,425 na vijijini kupitia mpango wa usambazaji umeme REA, wameweza kuwafikia wateja 1,187.

“Sisi hapa mikakati yetu mikubwa ni kupeleka umeme wa uhakika kwa wananchi hasa kule vijijini ili waweze kuwa na maendeleo, hivi sasa hata katika baadhi ya maeneo ambayo tayari nishati hii imewafikia wameweza kujenga mashine za kukoboa na kusaga nafaka ambazo zinatumia umeme”, alisema Punguti.

Akizungumzia juu ya upande wa matumizi ya nishati hiyo amewataka wateja watumie vizuri umeme huo kwa kufuata sheria za matumizi salama ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kutokea hapo baadaye na kwamba, shirika hilo limejipanga kuendelea kutoa elimu kwao juu ya usalama wa matumizi ya umeme na pale mteja anapokuwa na tatizo lolote asisite kuuliza au kutoa taarifa kwenye ofisi za TANESCO wilaya.

Vilevile aliongeza kwa kuwataka wateja hao kuepukana na vitendo vya wizi wa umeme majumbani kwani shirika hilo litaendelea kufanya ukaguzi kwa kila mteja ili kuweza kubaini kama kuna watu wamejiunganishia umeme kinyume na taratibu husika.

Alibainisha kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo hivi sasa ni uharibifu wa miundombinu ya umeme, ambapo wananchi hukata miti hovyo na kudondokea kwenye laini kuu za nguzo za umeme na huchoma misitu ambapo kufanya hivyo kunaathiri miundombinu hiyo.


Hata hivyo aliwaasa wananchi kuachana na vitendo hivyo badala yake walinde miundombinu hiyo na pale inapotokea hitilafu yoyote, watoe taarifa katika ofisi za vijiji au TANESCO wilaya ilipo karibu nao.

No comments: