Wednesday, January 4, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWASILI MKOANI RUVUMA ASISITIZA SERIKALI KUENDELEA KUNUNUA MAZAO YA WAKULIMA VIJIJINI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge mara baada ya kuwasili leo katika uwanja wa ndege Songea mkoani hapa kwa ziara ya kikazi, kulia kwake ni mke wa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mama Mahenge.
Na Mwandishi wetu,           
Songea.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwamba, serikali kupitia Wakala wake wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) itaendelea kununua mazao ya wakulima moja kwa moja vijijini, ili waweze kunufaika na bei elekezi ambayo imekuwa ikitolewa na serikali.

Majaliwa alisema hayo leo mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Ruvuma, Ikulu ndogo mjini hapa ambapo yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku tano hadi Januari 8 mwaka huu.

Alisema kuwa pamoja na serikali kutoa bei elekezi ya ununuzi wa mazao ya wakulima ambao ndio hasa wavuja jasho walikuwa hawanufaiki na bei hiyo nzuri, badala yake wafanyabiashara walanguzi ndio waliokuwa wakitajirika jambo ambalo kamwe haliwezi kupewa nafasi tena kwa sasa.

“Wananchi wanapaswa kuelekezwa juu ya umuhimu wa kutunza chakula walichokwishazalisha msimu uliopita, kutokana na uwepo wa kiwango cha mvua kisichoridhisha mwaka huu na maofisa kilimo katika halmashauri wawaelimishe wakulima hawa, namna ya kujikita zaidi katika uzalishaji wa mazao yanayostahimili ukame ili kukabiliana na uwezekano wa kutokea kwa njaa msimu ujao”, alisema Majaliwa.


Kadhalika Waziri Mkuu alifafanua kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kuikumba nchi ya Tanzania na dunia kwa ujumla wake, kwa kiasi kikubwa huchangiwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wananchi wenyewe ikiwemo ukataji hovyo wa miti, pengine kwa ajili ya kupanua mashamba au uchomaji wa mkaa kazi ambayo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa uoto asili wa misitu.

Alisema kuwa kila halmashauri ihakikishe kwamba inaandaa mpango mkakati wa utunzaji wa misitu ya asili iliyopo katika maeneo yao, na kwamba kwa kutekeleza hilo itasaidia pia katika kuviweka vyanzo vya maji katika hali ya usalama kwani navyo uhai wake hutegemea namna ambavyo mazingira yanavyotunzwa.

Vilevile akizungumzia juu ya masuala ya elimu, ameziagiza halmashauri za wilaya hapa nchini zihakikishe wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu, waripoti shuleni sambamba na watoto wote waliofikisha umri wa kuanza awali au darasa la kwanza waandikishwe na kupelekwa shule huku wazazi au walezi ambao wataonekana kutowapeleka watoto wao shule wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Majaliwa alisema kuwa serikali itaajiri walimu wa masomo ya sayansi kutokana na ukweli kwamba upungufu wa walimu hao ni mkubwa, ikilinganishwa na wale ambao wanafundisha masomo ya sanaa.

“Tulikuwa tumesimamisha ajira kutokana na kazi ya kuwaondoa watumishi hewa ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wakilipwa fedha nyingi huku wakiwa sio waajiriwa, lakini baada ya kukamilika kwa zoezi hili tutaanza kuajiri katika sekta ya afya na baadaye tutamalizia sekta ya elimu”, alisisitiza.

Pia alitoa onyo kali kwa maofisa utumishi ambao serikali itakapotoa kibali cha kuajiri, wataajiri watu ambao hawana sifa na kwamba wakurugenzi watapaswa kuhakikisha wanawasimamia maofisa rasilimali watu hao kwa umakini mkubwa kwani wao ndio hasa wanaoweza kuajiri watu wasiokuwa na sifa au la.


Pamoja na mambo mengine alisisitiza juu ya umuhimu wa kila halmashauri kuhakikisha vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na vyoo vinakamilika kwa shule zote za msingi na sekondari na kwamba suala la upungufu wa madawati, halipaswi kupewa nafasi kwani maelekezo yalikwishatolewa kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi kulisimamia jambo hilo kwa umakini mkubwa.

No comments: