Na Mwandishi wetu,
Songea.
KAYA masikini 260 kati
ya kaya 2,692 zilizoenguliwa katika Mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) wa kunusuru kaya maskini, katika Manispaa ya Songea mkoani hapa
zimeandika barua kupeleka Ofisi za TASAF makao makuu jijini Dar es Salaaam, kwa lengo la kukata rufaa juu ya
kuenguliwa kwao.
Ofisa habari wa Manispaa
hiyo, Albano Midelo alisema kaya hizo 2,692 kati ya kaya 7,695 zilizokuwa
zinanufaika na ruzuku hiyo zimeenguliwa baada ya uhakiki wa nyumba kwa nyumba
uliofanyika mwaka jana, ambapo baada ya uhakiki huo kaya zenye sifa zilibakia 5,003.
Midelo alieleza kuwa kati
ya kaya zilizoenguliwa ilibainika kuwa kaya 1,599 katika Manispaa ya Songea sio
masikini, kaya 342 walihama katika maeneo yao, kaya 110 walifariki, kaya 417
zilibainika kuwa ni hewa na kaya 144 hazikuwepo kwenye uhakiki huo.
Alisema kuwa mara baada
ya kaya zilizoenguliwa kupata barua ya kuondolewa kwao, yametokea malalamiko
mengi katika kaya hizo hali ambayo imesababisha Manispaa ya Songea kupita katika
mitaa ya walioenguliwa na kutoa elimu ya kukata rufaa kwa wale wanaodhani
wameonewa na wale ambao wametolewa kwa uhalali kuanza kulipa.
Kaimu Mratibu wa TASAF Manispaa
ya Songea, Mensa Ngerangera akitoa elimu kwa nyakati tofauti katika mitaa ya
Ruhuwiko kanisani, Ruhuwiko shuleni, Namanditi, Lilambo A na Sinai amewataka
wale wote ambao wametolewa kwa kukosa sifa waanze kulipa kama vile ilivyoelekezwa
kwenye barua.
Ngerangera alieleza kuwa
kaya maskini ambazo zimeondolewa kimakosa katika mpango huo zinatakiwa kukata
rufaa kwa kuandika barua TASAF makao makuu na kwamba ambaye hataandika barua ya
rufaa atatakiwa kuanza kulipa deni hilo.
Amezitaja sifa za kaya
zinazotakiwa kukata rufaa kuwa ni zile ambazo zinakula mlo mmoja kwa siku, kaya
isiwe na zaidi ya heka moja, asiwe mfanyabiashara, mstaafu wala mwenye mtoto au
ndugu wa karibu ambaye ni mtumishi wa umma na asiwe mwenye nyumba bora
iliyoezekwa kwa bati na kupiga sakafu.
Utafiti ambao umefanywa
katika baadhi ya mitaa ambayo wameenguliwa waliokuwa wanufaika, umebaini kuwa
kuna kaya ambazo zimeondolewa kwa makosa kwa kuwa zina sifa ya kaya maskini, ingawa
pia zipo kaya ambazo hazina sifa ya kaya maskini hivyo wanastahili kuenguliwa.
Ngerangera alisema
Novemba hadi Disemba mwaka jana kiasi cha shilingi milioni 277 zimetolewa kwa
kaya maskini ambazo zina sifa, katika mitaa 53 ya Manispaa ya Songea ambapo
Januari hadi Februari mwaka huu 2017 Manispaa hiyo itatoa kiasi cha shilingi milioni
256 kwa kaya maskini zenye sifa.
No comments:
Post a Comment