Dkt. Angelina Mabula, Naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
NAIBU Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Dkt. Angelina
Mabula ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
uhakikishe kwamba unatoa notisi kwa watu wote katika wilaya hiyo ambao hawajalipa
kodi ya ardhi, ili waweze kulipa kwa wakati uliopangwa na kwa wale ambao
watakaidi kulipa wapelekwe mahakamani.
Aidha alifafanua kuwa suala la kulipa kodi ya serikali ni
lazima na sio hiari na kwamba katika wilaya hiyo kuna jumla ya shilingi milioni
500 zipo nje kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi ambao wamemilikishwa viwanja kisheria
na hawataki kulipa kodi husika kwa wakati.
Agizo hilo lilitolewa jana na Dkt. Mabula wakati alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa, akizungumza na wananchi wa Mbinga na
viongozi wa wilaya kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
Dkt. Mabula alisisitiza pia katika kupunguza kero na migogoro
ya ardhi ni vyema sasa viongozi husika ambao wamepewa dhamana ya kushughulikia
masuala ya ardhi, wawafikie wananchi mara kwa mara kwenye maeneo yao na kutatua
matatizo hayo yaliyopo kwa wakati.
“Pangeni ratiba mbalimbali ya kuwafikia wananchi pale walipo,
tukifanya hivyo tutaweza kupunguza kero na migogoro hii ambayo inaleta usumbufu
katika jamii na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa hili”, alisema.
Vilevile aliutaka uongozi wa wilaya ya Mbinga kuwalipa fidia wananchi
wote ambao hawajalipwa fidia zao mara baada ya kutwaliwa viwanja vyao na kwamba
kwa wale pia ambao wanadai hati miliki za viwanja vyao wapewe kwa wakati ili
kuondoa migogoro na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
“Hakikisheni hati zote za kawaida na kimila zinatolewa kwa
wakati na pia wananchi wale ambao hawajapata hati zao nawashauri kama wana ofa
zipelekeni halmashauri ili muweze kupata hati zenu na pale panapotakiwa kulipa
gharama husika lipeni ili muweze kupata hati zenu”, alisisitiza Dkt. Mabula.
Pia aliwataka viongozi wa wilaya wahakikishe wanatenga maeneo
ya kuchungia mifugo ili kuepukana na migogoro ya ardhi, watu kupigana na
kupoteza maisha jambo ambalo hatimaye linapoteza nguvu kazi ya taifa hili.
Kadhalika aliongeza kwa kuwataka wananchi waache vitendo vya
kuharibu mazingira ya vyanzo vya maji na kuchoma moto misitu kwani kufanya
hivyo kunaweza kusababisha kukosa mvua na kukaribisha hali ya ukame.
Hata hivyo katika ziara hiyo ya Naibu Waziri Dkt. Mabula
aliweza kusikiliza kero na migogoro mbalimbali kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga
na kuweza kuipatia ufumbuzi kwa kuwataka viongozi waliopewa dhamana ya
kusimamia masuala ya ardhi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi
na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment