Na Julius Konala,
Mafia.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani, imejiwekea
mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara wilayani humo
kutoka zao moja la nazi linalozalishwa sasa, hadi kufikia matatu ikiwemo zao la
korosho kwa lengo la kuinua pato la halmashauri hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Erick Mapunda alisema
hayo juzi alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake wilayani Mafia kwa
lengo la kuelezea shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na halmashauri
hiyo.
Aidha Mapunda alisema kuwa mpaka sasa tayari wamekwisha tenga
kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia kilo 200 za mbegu ya korosho, ambapo zitaweza
kuzalisha miche 1000 ambayo itagawiwa bure
kwa wananchi na taasisi za shule.
Vilevile alisema halmashauri yake pia ina mpango wa kuzalisha
zao la mbaazi ambalo litasaidia kuchangia kwa kiasi kikubwa kuinua pato la
halmashauri pamoja na uchumi wa mtu mmoja mmoja katika wilaya hiyo.
“Ndugu mwandishi wa habari ninachotaka kukueleza hapa ni
kwamba halmashauri yetu imekuwa nyuma kimapato kutokana na kutegemea makusanyo
yake ya ushuru kwenye zao moja tu la biashara ambalo ni nazi za asili ambazo huzalishwa
tani 35,000 kwa mwaka, pamoja na uvuvi ambapo makusanyo yake ni madogo jambo
ambalo linatufanya tushindwe kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo ya
wananchi kutokana na kukosa vyanzo vingine vya mapato”, alisema Mapunda.
Katika kukabiliana na hali hiyo alisema kuwa halmashauri ina
mpango wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya upandaji miti mipya ya mikorosho, mbaazi
pamoja na upimaji wa viwanja na walengwa kupewa hati miliki kwa lengo la kuinua
pato la halmashauri, kukuza uchumi wa wananchi na kuondoa makazi holela
Pamoja na mambo mengine alizitaja changamoto anazokumbana
nazo kuwa ni wananchi kutoshiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo
hususani katika suala la upandaji wa miti mipya ya mikorosho na badala yake
wamekuwa waking’ang’ania ile ya zamani ambayo haiwaletei tija.
No comments:
Post a Comment