Wednesday, January 25, 2017

BENKI YA CRDB KUWAFUNGULIA MASHTAKA MBINGA KURUGENZI SACCOS

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

MENEJA Mahusiano wa benki ya CRDB Kanda ya Nyanda za juu kusini, Hassanaly Japhary amesema kuwa ameshangazwa na kauli ya Wajumbe wa bodi ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS, kwamba hawazitambui baadhi ya nyaraka za benki hiyo ambazo zilitumika kuwapatia mkopo wa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuwakopesha wanachama wa ushirika 

Alifafanua kuwa kauli hiyo ya kushangaza ilitolewa na Wajumbe hao katika mkutano wao maalumu uliofanyika mjini hapa na kwamba benki hiyo, haipo tayari kuchafuka kwa mambo hayo badala yake itafungua mashtaka dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za mkopo huo, yaliyofanywa na Wajumbe hao kwa kujinufaisha wao binafsi badala ya kuwakopesha wanachama wa SACCOS hiyo.

Hassanaly alisema hayo juzi alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kusomwa taarifa ya ukaguzi juu ya mwenendo wa Chama hicho cha ushirika ambayo ilibainisha wizi wa fedha zilizotokana na mkopo huo shilingi milioni 405,204,514 katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama, uliofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

“Benki hatupo tayari kuchafuka kwa mambo haya, sisi kama benki nasi tutahakikisha tunafungua mashtaka mahakamani dhidi ya wizi huu uliofanyika hapa Mbinga katika SACCOS hii ili tuweze kurejesha fedha zetu”, alisisitiza Hassanaly.


Pia alisema kuwa leo hii haiwezekani baadhi ya watendaji na wajumbe wa bodi hiyo wanasema hawazitambui baadhi ya nyaraka za benki hiyo kutokana na ujanja walioufanya wakujikopesha fedha wenyewe badala ya wanachama jambo ambalo ni kinyume na utaratibu waliopewa.

Kadhalika aliongeza kuwa benki haitakuwa na msamaha katika hili hivyo wanachopaswa ni kurejesha fedha zote walizochukua vinginevyo riba itazidi kuongezeka kadiri ya mkopo huo wanavyochelewa kuulipa na wakati huo taratibu za kisheria zitaendelea kuchukua mkondo wake.

Awali wizi wa fedha hizo ulibainishwa na Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma, Biezery Malila ambapo watumishi saba wanaotoka katika halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani humo, ambao pia ni Wajumbe wa bodi ya Chama hicho cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS ndio wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha hizo na kwamba wamekamatwa na bado mpaka sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Mrajisi huyo pia alimtaja mtuhumiwa mwingine wa nane ambaye sio mtumishi wa serikali kuwa ni Meneja wa SACCOS hiyo, Raymond Mhagama ambapo ametoroka kufuatia kuwepo kwa kesi ya ubadhirifu wa fedha hizo na madai yake ya kutoroka huko yamefunguliwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na kwamba, anatafutwa popote pale alipo ili aweze kukamatwa na kujibu tuhuma hizo zinazomkabili mbele yake.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alipohojiwa na mwandishi wetu aliwataja watumishi hao saba waliowekwa mahabusu mpaka sasa kuwa ni Zackaria Lingowe, Emmanuel Mwasaga na Alex Kalilo ambao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jamima Challe na Stella Mhagama wanatoka halmashauri ya mji wa Mbinga, Lucas Nchimbi na Mhadisa Meshack nao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga na kwamba mpaka sasa bado wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakiendelea kuhojiwa zaidi kutokana na tuhuma zinazowakabili ili waweze kufikishwa Mahakamani.

No comments: