Na Kassian Nyandindi,
Songea.
VIONGOZI wa serikali mkoani Ruvuma, wameagizwa wahakikishe
kwamba watoto wote walioandikishwa kuanza elimu ya awali, msingi na sekondari
kwa mwaka huu wa masomo wanakuwepo shuleni mara shule zitakapofunguliwa Januari
9 mwaka huu.
Kadhalika wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya watoto wenye umri
wa kwenda shule ambao hivi sasa, wamekuwa wakishinda kwenye vituo vya mabasi (Magari
ya abiria) ili waweze kwenda shule na kuweza kumaliza kabisa tatizo la utoro
katika mkoa huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa agizo hilo leo akiwa mkoani
Ruvuma katika ziara yake ya siku nne mara baada ya kupokea taarifa ya
maendeleo ya mkoa iliyosomwa na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge Ikulu
ndogo mjini Songea.
Amewaonya Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na miji hapa
nchini kutekeleza kwa kusimamia kikamilifu mpango wa utoaji wa elimu bure kwa
shule za serikali, ambao unatoa nafasi kwa vijana wengi zaidi kupata fursa ya
kusoma kwani serikali imeshaondoa gharama zote ambazo zilikuwa kikwazo kwa
baadhi ya familia.
Pamoja na agizo hilo Waziri Mkuu, Majaliwa ameagiza pia
jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwenye maeneo yao ili waweze
kuepuka hatari ya kutokea ukame hasa ukizingatia kuwa mkoa wa Ruvuma, unafaa
kwa shughuli za kilimo na ni moja kati ya mikoa inayopata mvua za kutosha mwaka
hadi mwaka.
Alisema kuwa suala la utunzaji mazingira sio la hiari bali ni
la lazima kwa kila mmoja wetu, kuhakikisha anawajibika katika
kutunza mazingira yanayomzunguka kwenye eneo lake kwa faida ya kizazi cha sasa
na kijacho na iwe ajenda ya mara kwa mara watendaji
wa serikali pamoja na viongozi kuzungumzia jambo hilo pale wanapokutana na
wananchi.
“Viongozi kila mnapokutana na wananchi jambo la kwanza ni
lazima muwaeleze umuhimu wa kutunza mazingira yetu hali hii ninayoiona leo hapa
Ruvuma, kwa kweli inaniogopesha sana kwani kawaida mwezi kama huu wakulima
wengi wanakuwa wameshapanda lakini mwaka huu ni tofauti kabisa”,
alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Akizungumzia kuhusiana na shughuli za madini Waziri
Mkuu aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji katika suala
zima la utafutaji na uchimbaji katika maeneo mbalimbali ya nchi, ili madini hayo
yatakayopatikana yaweze kusaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi na kukua
kwa pato taifa.
Vilevile aliziagiza mamlaka husika Ofisi ya madini Kanda ya
Songea kupitia upya leseni zote za madini ili kuepusha migogoro kati ya
wawekezaji wakubwa na wachimbaji wadogo kama ilivyowahi kutokea katika maeneo
mengine jambo linapaswa kudhibitiwa mapema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu huyo amewataka watendaji na
wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuendelea na ukusanyaji mapato katika
halmashauri zao kwa kutumia mfumo wa mashine za EFD’S katika kukusanya mapato
hayo ili kuepuka wizi na badala yake itasaidia kujenga udhibiti mapato yatakayopatikana.
Pia ameagiza kuwepo na matumizi sahihi ya fedha hizo zinazopatikana
na kuhakikisha kwamba kila zinapokusanywa zinapelekwa benki kwa usalama zaidi
badala ya kuwachia watu wanaokusanya ambao wanaweza kuzichezea au kuzielekeza
katika matumizi mengine.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amerudia agizo lake la kufuta
posho kwa watumishi wa umma na madiwani badala yake ameelekeza fedha ambazo
zilikuwa zikitumika kwa ajili ya kulipana posho, sasa zielekezwe
katika miradi ya maendeleo ya wananchi ili kusaidia kuboresha huduma mbalimbali
za kijamii katika maeneo yao.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inaendelea
kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa wa Ruvuma kwa kiwango cha lami, ili
Watanzania waweze kusafiri kwa uhakika na kufanya shughuli zao za kiuchumi
badala ya kutumia muda mrefu kusafiri katika barabara za vumbi.
“Baada ya kukamilika kwa barabara ya lami kutoka Songea hadi Tunduru
kupitia wilaya ya Namtumbo kwenda Masasi mkoa wa Mtwara mpango wa baadaye wa
serikali ni kujenga barabara ya lami kutoka Nachingwea, Rwangwa hadi Dar es Salaam
kupitia Nangurukuru wilayani Kilwa barabara ambayo itapunguza umbali wa kutoka
Songea kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine.
Pia Waziri Mkuu amewahakikishia wananachi wa mkoa wa Ruvuma
kwamba, serikali ipo katika hatua ya mwisho kukamilisha mchakato wa kuanzisha
safari za ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Songea kwa kutumia ndege za shirika
la ndege nchini ATCL.
No comments:
Post a Comment