Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
MGOMO wa wakulima wanaozalisha mazao ya aina mbalimbali
katika kijiji cha Namabengo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, umepatiwa ufumbuzi na Mkuu wa wilaya hiyo Luckness Amlima
baada ya kwenda kijijini hapo kusikiliza madai yao na kuyapatia majawabu.
Madai hayo yaliyopatiwa ufumbuzi yalikuwa pamoja na wakulima
hao kukataa kununua mbegu za ruzuku ya serikali kwa madai kuwa mbegu hizo,
zimechelewa kuwafikia ambapo wananchi katika msimu wa mwaka huu tayari
wamepanda katika mashamba yao kwa kutumia mbegu za asili walizokuwa nazo.
Vilevile baada ya kufikia muafaka juu ya jambo hilo, wakulima
waliachiwa baadhi ya mbegu pamoja na mbolea za kukuzia huku wakiitaka serikali msimu
ujao kupeleka pembejeo mapema ili isiweze kutokea tena hali kama hiyo.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya, Amlima aliwataka wananchi
kuzingatia utaratibu uliowekwa na serikali wa kuchukua mbolea za kupandia na
kukuzia pamoja na mbegu ambazo tayari zimewekewa ruzuku.
Kadhalika madai ya wananchi hao kuchelewa kupata pembejeo
hizo yanatokana baada ya serikali kubadilisha utaratibu ule wa awali, ambao
ulizoeleka ambapo mawakala walikuwa wakiteuliwa kuzisambaza kwa wakulima na
kusababisha kutowafikia walengwa.
Ambapo hivi sasa makampuni ndiyo yanayosambaza pembejeo hizo
za kilimo kwa lengo la kupunguza malalamiko ya kutowafikia wananchi pembejeo, ili
waweze kunufaika na ruzuku ya serikali na sio kwa wajanja wachache.
Naye kwa upande wake Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Stephen
Mtunguja aliongeza kuwa msimu huu wa kilimo pamoja na mvua kuchelewa kunyesha
lakini wakulima wanapaswa kuongeza jitihada ya kuzalisha mazao kwa wingi, ili
kuweza kuondokana na matatizo ya njaa yanayoweza kujitokeza katika msimu ujao.
No comments:
Post a Comment