Tina Sekambo Mkurugenzi Manispaa ya Songea. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa mkopo
wa shilingi milioni 72.5 ambazo zimetokana na mapato yake ya ndani kwenda katika
vikundi vya wanawake na vijana ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Mkopo huo umetolewa katika kipindi cha mwaka jana kwa awamu
mbili ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya shilingi milioni 52.5 zilikopeshwa
kwenye vikundi hivyo.
Aidha kati ya fedha hizo vikundi 73 vya wanawake vilikopeshwa
zaidi ya shilingi milioni 36 na vikundi 35 vya vijana vilikopeshwa shilingi milioni
16.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano
Midelo alisema kuwa katika awamu ya pili Manispaa imetoa mkopo wa shilingi milioni
20 kwa vikundi ambapo vikundi vya wanawake 32 vilipewa shilingi milioni 15.4 na
vikundi 10 shilingi milioni 4.6.
Alisema vikundi hivyo vimetoka katika kata 21 zilizopo katika
Manispaa hiyo na kwamba mikopo iliyotolewa ni kati ya shilingi laki sita hadi
nane kwa kila kikundi ambazo wanatakiwa kurejesha baada ya miezi 12 ili waweze
kukopeshwa wengine kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za ujasiriamali.
Kwa ujumla Manispaa ya Songea imekuwa ikitoa mikopo hiyo kwa riba
ya asilimia kumi tu kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo asasi nyingi za kifedha
zimekuwa zikitoa riba kubwa yenye makato mengi hali inayosababisha wakopaji wengi
wenye kipato kidogo kushindwa kufikia malengo yao.
Mkopo huo unatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali vya
wanawake na vijana kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1993 ambayo imeagiza kutoa
mkopo kwa kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri husika, lengo ikiwa
ni kuinua hali ya uchumi katika makundi hayo mawili.
No comments:
Post a Comment