Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimewataka wananchi
wa kata ya Maguu wilayani Mbinga mkoani hapa, kumchagua mgombea
anayetokana na chama hicho katika uchaguzi wa nafasi ya udiwani unaotarajiwa
kufanyika Januari 22 mwa huu.
Akizungumza juzi na wananchi wa kata hiyo katika
uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zilizofanyika katika viwanja
vya michezo mji mdogo wa Maguu Mwenyekiti wa CCM wa mkoa hu, Oddo Mwisho
alisema kuwa wanachama na wananchi kwa ujumla wake wanapaswa kukiamini chama
hicho kwa kuwa ndicho pekee chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi
wake.
Mwisho alisema kata hiyo ilikuwa mikononi mwa CCM hivyo
wananchi wanakila sababu ya kuendelea kukiamini na kwamba vyama vya
upinzani havipaswi kupewa kuongoza kata hiyo kutokana na kukosa historia ya
kuwatumikia wananchi ipasavyo katika kuwaletea maendeleo kwenye maeneo yao
wanayoishi.
“Ndugu zangu wananchi kumbukeni jinsi ambavyo majimbo na kata
ambazo vyama vya upinzani wamepata nafasi ya kuongoza wameshindwa kuwaletea
maendeleo, kila kukicha wao kazi yao kubwa ni kuhamasisha maandamano ya kupinga
mambo ambayo yanatekelezwa na serikali ya chama tawala”, alisema.
Kwa upande wake mgombea Manfred Kahobela akiomba ridhaa kwa
wanachama wake na wananchi wakati wa uzinduzi huo alisema kuwa, endapo kama
atachaguliwa atahakikisha anatekeleza majukumu yake ya kujenga ushirikiano nao
katika kufanya shughuli za maendeleo na kwamba zile ahadi zilizoachwa na
mtangulizi wake atazipatia kipaumbele na sio vinginevyo.
Kahobela alisema anafahamu changamoto mbalimbali ambazo
wananchi wa kata hiyo wanakabiliana nazo hivyo kinachotakiwa sasa wananchi
ambao ni wapiga kura katika kata hiyo, wahakikishe ifikapo Januari 22 mwa huu wanamchagua ili aweze kuzipatia ufumbuzi wa kudumu katika kuwaletea maendeleo
wananchi wake.
Uchaguzi huo mdogo unafanyika kufuatia diwani wa kata hiyo ya
Maguu Nathaniel Hyera kufariki dunia kutokana na kuugua ugonjwa wa shinikizo la
damu, ambapo alifikwa na mauti Marchi 8 mwaka jana wakati akipatiwa
matibabu katika hospitali ya wilaya Mbinga mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment