Na Mwandishi wetu,
Songea.
CHAMA cha Waganga wa jadi, wakunga na mangariba wa tiba asilia
mkoani Ruvuma (CHAWATASO) kimetoa rai kwa serikali kuweka sheria kali itakayoweza
kuwadhibiti watu wanaochoma misitu na kukata miti hovyo.
Mwenyekiti wa chama hicho, Mustafa Kafimbo amesema kuwa
endapo hatua zisipochukuliwa za kudhibiti vitendo hivyo vya uharibifu wa misitu
hali hiyo itasababisha miti mingi iliyokuwa ikitumika kutengenezea dawa kupotea
na kuwa kero katika jamii.
Kafimbo ameiomba pia serikali kukitambua chama chao ambacho
kilisajiliwa mwaka 2008 na kupewa namba ya usajili 17NGO/0441 kikiwa na jumla
ya wanachama waanzilishi 13 mkoani hapa ambapo hivi sasa chama hicho kina
wanachama 348.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kutokana na kuongezeka kwa
vitendo vya uharibifu wa mazingira, kinaiomba serikali kukipatia chama hicho pia
ardhi kwa ajili ya kupanda miti ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa mvua
ambalo linatokana na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Katibu wa CHAWATASO mkoani Ruvuma, Mayasa
Mfaume naye alieleza kuwa chama hicho kimeendelea kutoa huduma ya tiba asilia kwa
umakini mkubwa na kwamba kimekuwa pia kikipambana na kupinga vitendo vya uchawi
na ramli chonganishi.
Mayasa amezitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni baadhi ya
vyama vya tiba asilia kujiona ni bora zaidi na kuanza vitendo vya kuwanyanyasa
baadhi ya wanachama wa chama hicho kwa kuwanyang’anya tiba zao na kutozwa
michango ambayo haitambuliki.
“Jamii inawategemea CHAWATASO katika masuala ya kujenga afya zetu
kwa kutumia tiba mbadala, naomba endeleeni kuwa mabalozi wa kuhamasisha mila na
desturi kwa kuwa katika kipindi hiki cha utandawazi vijana wengi wanadharau
utamaduni wetu na kuiga utamaduni wa kigeni’’, alisema Mbawala.
Hata hivyo katibu huyo wa Mbunge wa Songea mjini ameahidi
kutafutia ufumbuzi matatizo yote yanayoikabili chama hicho yakiwemo ya
kunyanyaswa kwa baadhi ya wanachama wake ili yaweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu
na hatimaye waweze kufanyakazi kwa amani na utulivu.
No comments:
Post a Comment