Na Kassian Nyandindi,
Songea.
PATO la Mwananchi wa kawaida hapa nchini (Percapital income)
katika mkoa wa Ruvuma limepanda kutoka shilingi milioni 2,082,167 mwaka juzi hadi
kufikia shilingi milioni 2,415,485 kwa mwaka 2016, hatua ambayo imeufanya mkoa
huo kushika nafasi ya tatu kitaifa ikitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam
na Iringa.
Aidha pato hilo linaonesha kwamba ni ongezeko la asilimia 16
ikilinganishwa na pato la mtu mmoja kwa mwaka 2014 ambapo ongezeko
hilo limetokana na shughuli ya kiuchumi kama vile kilimo ambacho hutegemea kwa
kiasi kikubwa wakazi wa mkoa huo kuendeshea maisha yao.
Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith
Mahenge alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya mkoa huo kwa Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa Ikulu ndogo mjini Songea.
Dkt. Mahenge alisema kuwa wananchi wake hutegemea shughuli
hizo kiuchumi ambapo zaidi ya asilimia 87 ya wakazi wake, hupata riziki yao kutokana
na shughuli hiyo ambayo huchangia pia pato la taifa kwa asilimia 3.3 kwa mwaka,
huku pato la mkoa likifikia wastani wa asilimia 75.
Alifafanua kuwa mkoa wa Ruvuma, unafursa nyingi ambazo hutumiwa
katika kusukuma mbele maendeleo ya mkoa ambapo eneo kubwa la mkoa huo linafaa
kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji na kuufanya mkoa kuwa ni miongoni
mwa mikoa michache yenye bahati ya kupata mvua za kutosha ambazo hunyesha
kuanzia mwezi Novemba hadi Mei kila mwaka.
Mkuu huyo wa mkoa alielezea kuwa kufunguka pia kwa miundombinu
ya barabara inayounganisha makao makuu ya mkoa na wilaya zake, pamoja na mikoa
mingine imesaidia kwa kiasi kikubwa kuharakisha kukua kwa shughuli za kiuchumi
katika mkoa wa Ruvuma.
Alisema kuwa malengo ya kilimo katika msimu wa mwaka
2015/2016 mkoa ulilenga kulima jumla ya hekta 892,525 za mazao ya chakula na
biashara zilizotarajiwa kutoa mavuno tani 2,377,004 ambapo mazao ya chakula
ilitarajiwa kulimwa hekta 637,663 zilizotarajiwa kutoa mavuno tani
1,939,946 na mazao ya biashara ilitarajiwa kulimwa hekta 254,862 na
kutoa mavuno tani 437,058.
Vilevile utekelezaji wa malengo hayo hadi kufikia mwezi Juni
mwaka jana, mkoa huo ulikwisha zalisha hekta 877,035 sawa na asilimia 98.3 ya
lengo lililowekwa ambalo lilikuwa ni kuzalisha jumla ya hekta 892,525 zilizotoa
mavuno tani 2,127,180 sawa na asilimia 89.4.
Pia alibainisha kuwa kati ya hekta hizo za kilimo cha mazao
ya chakula jumla zililimwa hekta 703,709 ambazo zimetoa mavuno ya tani
1,955,424 na kwamba katika kilimo cha mazao ya biashara hekta zilizolimwa ni
173,326 na zilitoa jumla ya hekta 171,756 za mavuno yote.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Majaliwa alipongeza jitihada
hizo zinazofanywa na viongozi wa mkoa wa Ruvuma ikiwemo kukua kwa pato hilo la
mwananchi wa kawaida, huku akisisitiza kuwa zisiishie hapo wanachopaswa ni
kuendelea kuhamasisha wananchi wazalishe mazao ya chakula na biashara kwa wingi
ili waweze kuondokana na umaskini.
No comments:
Post a Comment