Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa ameagiza Halmashauri zote za wilaya hapa nchini zitambue vyanzo vyote
vya maji na hatimaye vitunzwe na kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Aidha Majaliwa amesema kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano
ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji safi na salama, hivyo hawana
budi kuwa na tabia ya kutunza vyanzo hivyo kwa manufaa ya jamii.
Majaliwa alisema hayo leo wakati alipokuwa akifungua mradi wa
maji wa vijiji vya Mkongotema na Magingo wilaya ya Songea vijijini mkoani
Ruvuma, ambao ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.9 na wenye
uwezo wa kuhudumia wakazi 5,300 wanaoishi katika maeneo hayo.
Alisema kuwa ili mradi huo uweze kuwa endelevu wananchi
katika maeneo mengine ambako miradi kama hiyo inatekelezwa, wanapaswa kujenga
tabia ya kuchangia miradi yao ya maendeleo hasa pale inapojengwa ili iweze
kukamilika kwa wakati.
“Maeneo ambayo wananchi wamekuwa hawachangii miradi ya
maendeleo huwa inakwama ujenzi wake na haikamiliki kwa wakati na ili miradi hii,
iweze kudumu kwa muda mrefu wananchi wanapaswa kujenga tabia ya kutunza vyanzo
vya maji”, alisisitiza Majaliwa.
Pia alieleza kuwa wananchi waache tabia ya kuchoma moto hovyo,
kukata miti, kulima na kuingiza mifugo karibu na vyanzo hivyo badala yake
wapande miti rafiki ya maji kwa wingi ili kuweza kutunza uoto wake wa asili.
Katika kufanikiwa hilo, amesisitiza juu ya umuhimu wa
uundwaji wa kamati za maji vijijini ambazo zitakuwa na wajibu wa kusimamia
vyanzo vya maji na miundombinu mingine ya maji katika eneo husika ikiwemo kuhakikisha
kwamba matumizi ya maji yanakuwa sahihi wakati wote.
No comments:
Post a Comment