Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo katika sehemu ya vikao vyake vya kikazi na chama mkoani hapa. |
Na Julius Konala,
Songea.
WATUMISHI wa Serikali waliopo katika sekta mbalimbali mkoani
Ruvuma, wametakiwa kujiepusha na vitendo vya utoaji huduma kwa wananchi kwa
mtindo wa upendeleo au kujenga tabia ya kuendekeza vitendo vya rushwa, itikadi
za dini na ukabila.
Aidha kwa mtumishi yeyote atakayebainika kufanya hivyo
atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi, ili iweze kuwa fundisho
kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema hayo
juzi alipokuwa akizindua Baraza la Wafanyakazi la watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu
wa mkoa huo lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Ikulu ndogo mjini Songea.
Dkt. Mahenge alieleza kuwa serikali haitasita kumchukulia
hatua za kinidhamu mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume cha sheria, taratibu
na kanuni za utumishi wa umma badala yake wanapaswa kuwahudumia Watanzania wote
kwa kufuata usawa.
“Nawataka watumishi wote ndani ya mkoa wangu endeleeni kuunga
mkono kauli mbiu ya Rais wa awamu ya tano Dkt. John Magufuli ya Hapa kazi tu, kwa
kufanya kazi kwa bidii, weledi na maarifa acheni kutumia muda mwingi mnapokuwa
ofisini kuchati kwenye mitandao badala ya kufanya kazi, malizeni kero za
wananchi kwa wakati”, alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la
watumishi wa Ofisi hiyo ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko ambaye pia
ni Katibu tawala wa mkoa huo alisema kuwa lengo la kuundwa kwa baraza hilo ni
kuboresha utendaji kazi, mahali pa kazi na kuzungumzia changamoto mbalimbali
zinazowakabili watumishi wa umma ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka na wa
kudumu.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo Katibu wa Chama Cha
Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) mkoani Ruvuma, Denice Tosiri
aliwataka wajumbe wa baraza hilo kutambua kuwa wajibu wao mkubwa ni kutoa
changamoto, kuzungumzia kero, kuwepo kwa ushirikiano kati ya watumishi na
waajiri, kuishauri serikali juu ya ufanisi mahali pa kazi, kuboresha maslahi
yao kazini, kupandishwa vyeo na kutoa ushauri katika matumizi ya fedha.
Tosiri aliongeza kuwa wajumbe hao wanatakiwa pia kutambua kuwa wao ni mabalozi wanaowakilisha wenzao, hivyo pale wanaposikia manung’uniko na migogoro sehemu za kazi wanapaswa kutatua haraka iwezekanavyo huku wakitakiwa kuboresha huduma kwa wateja, kuonyesha nidhamu pamoja na kutunza siri za ofisi.
No comments:
Post a Comment