Na Muhidin Amri,
Songea.
WAJASIRIAMALI wadogo na wakati kutoka katika wilaya tano za
mkoa wa Ruvuma, wameipongeza benki ya NMB kwa kuwa na mipango thabiti
inayolenga kupunguza umaskini kwa wananchi wengi, ikiwemo kutoa mikopo yenye
riba nafuu hatua ambayo itasaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi.
Pongezi hizo zilitolewa na Wajasiriamali hao wa kutoka wilaya
ya Tunduru, Namtumbo, Mbinga, Songea na Nyasa mkoani humo wakati walipokuwa
juzi kwenye kikao chao na uongozi wa benki hiyo Kanda ya kusini, kinachojulikana
kwa jina la NMB BUSINESS CLUB ambacho kilihudhuriwa pia na maafisa kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania, Jeshi la zimamoto na Maafisa biashara wa Manispaa
ya Songea katia ukumbi wa Heritage Cottage mjini hapa.
Aidha wameiomba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt.
John Magufuli kuiunga mkono benki hiyo ambayo imeonekana kuwa mkombozi mkubwa
kwa wananchi wengi, hasa wenye kipato kidogo ambao wameanza kunufaika na huduma
mbalimbali zinazotolewa na benki ya NMB ikiwemo zile za mikopo ambayo huwawezesha
kuanzisha biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine za kimaendeleo.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajasiriamali hao
wilayani Songea wameuomba uongozi wa Manispaa ya Songea kuondoa kiwango
cha fedha inachotoza kwa wananchi wanaotaka kuchukua mkopo na
kutumia hati zao za nyumba kama dhamana ambazo hupelekwa idara ya ardhi kwa
ajili ya uhakiki kwani tozo hizo humuumiza mwananchi wa kawaida na kukwamisha
malengo yake.
Walisema kuwa Manispaa hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikiwatoza wananchi
shilingi 40,000 kila anayehitaji kupata mkopo kutoka benki au taasisi yoyote
ile ya kifedha jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa kwani mtu anapohitaji mkopo
benki ni lazima alipie fedha hizo.
Walifafanua kuwa utaratibu huo haufai na kwamba hauwezi kumsaidia
mwananchi wa kawaida kumuondoa katika janga la umaskini, badala yake wameshauri
Manispaa kutafuta vyanzo mbadala vya mapato kuliko kuendelea kuwanyonya watu
maskini wanaokabiliwa na changamoto nyingi za maisha.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Sara Komba alisema kuwa
kuna umuhimu sasa kwa serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuachana
na vile vinavyomuumiza mwananchi ambaye hutafuta namna ya kujikwamua na
umaskini.
Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB tawi la Songea, Colman
Kiwia alisema kuwa licha ya mafanikio makubwa iliyoyapata benki hiyo hata
hivyo kuna changamoto kubwa iliyopo kutoka kwa baadhi ya wateja
wanaochukua mikopo kushindwa kuirejesha kwa wakati na waombaji wapya kukosa
sifa ya kupata mkopo pale wanapotaka kutumia ardhi zao ambazo hazijapimwa kutokana
na kukosekana kwa hati miliki.
Hata hivyo alisema kuwa wakati umefika sasa kwa wananchi wa
Songea kuona umuhimu wa kupima maeneo yao ili waweze kupata hati hizo
miliki, ambazo zitawasaidia kwa ajili ya kupata mikopo kutoka katika
taasisi za kifedha na kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali za
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment