Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) halmashauri
ya mji wa Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetakiwa ihakikishe kwamba huduma ya
upatikanaji wa maji safi na salama katika mji huo inatosheleza wakati wote kwa
ajili ya matumizi ya wananchi.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt.
Binilith Mahenge alipokuwa akizungumza na wakuu wa idara wa wilaya hiyo katika
kikao cha kazi kilichofanyika mjini hapa.
“Nataka kuona maji yanatosheleza katika mji huu ili tuweze
kuwaondolea adha wananchi wetu kutafuta maji umbali mrefu, boresheni mindombinu
ya maji na kukusanya madeni ya ankra za maji kwa wakati”, alisisitiza Dkt.
Mahenge.
Mkuu huyo wa mkoa aliagiza pia kwa kuutaka uongozi wa Mamlaka
hiyo kutunza vyanzo vyake vya maji kwa kuwaondoa watu wote waliovamia vyanzo
hivyo, ili visiweze kukauka na kuleta madhara makubwa ya kutopatikana maji ya kutosha
katika mji huo.
Alisema anataka kuona mkoa wa Ruvuma katika maeneo mbalimbali
mazingira yanatunzwa vizuri ili uoto wa asili uliopo sasa, uweze kuwa endelevu
kwa faida hata ya viumbe hai ambavyo huishi katika misitu na maeneo mengine.
“Tunataka mkoa wetu wananchi waheshimu suala la utunzaji wa
mazingira, vinginevyo pale nitakapoona kuna tofauti fulani viongozi wa wilaya
jambo hili litawagharimu”, alisema.
Hata hivyo Dkt. Mahenge alikemea vitendo vya ukataji miti
hovyo na uchomaji moto misitu hiyo ambapo amewataka viongozi husika, kusimamia
jambo hilo kwa kuhakikisha watu hawafanyi uharibu huo ili mazingira yasiweze
kuharibiwa na kuleta madhara makubwa hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment