Wednesday, September 14, 2016

RC RUVUMA APONGEZA UFYATUAJI TOFARI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akishiriki na wananchi katika zoezi la ufyatuaji tofari katika kata ya Nyoni wilaya ya Mbinga mkoani humo.
Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amewapongeza wananchi kata ya Nyoni wilayani Mbinga mkoani humo kwa jitihada wanazozifanya za ufyatuaji wa matofari kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu na zahanati ya kijiji cha Likwera zilizopo katika kata hiyo.

Dkt. Mahenge alitoa pongezi hizo juzi wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, kukagua miundombinu ya ujenzi wa barabara na maendeleo mbalimbali yanayofanywa na wananchi wa wilaya hiyo.

“Nawapongeza wananchi wa kata hii ya Nyoni kwa moyo huu mlionao wa kujitolea katika shughuli za maendeleo nawaomba endeleeni kufanya hivi, ili tuweze kufikia malengo ya kuwa na nyumba za kutosha za walimu na zahanati zetu za kutolea huduma ya afya kwa kila kijiji”, alisema Dkt. Mahenge.


Vilevile Dkt. Mahenge aliuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo wananchi watakapoanza kufanya kazi ya ujenzi inunue na kuwapatia vifaa vya kiwandani ili waweze kukamilisha ujenzi wa majengo hayo, kabla mvua hazijaanza kunyesha katika msimu wa mwaka huu ili tofari walizozifyatua zisiweze kuharibika.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya kata hiyo mbele ya Mkuu huyo wa mkoa huyo, Ofisa mtendaji wa kata ya Nyoni Husna Chiponda alimweleza Mkuu wa mkoa Dkt. Mahenge kuwa tayari wananchi wamefyatua tofari 20,500 kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi huo.


Chiponda alifafanua kuwa mpaka sasa pia wanabenki tofari 70,000 ambazo tayari zimechomwa kwa ajili ya kuweza kuanza kazi ya ujenzi huo na kwamba wananchi wanaendelea kuhamasishwa ili kuweza kukamilisha kazi ya ufyatuaji wa matofari hayo na ujenzi wa nyumba za walimu pamoja na zahanati.

No comments: