Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATUMISHI wa serikali katika mkoa wa Ruvuma, wametakiwa
kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wanapaswa kuendana na kasi ya
serikali ya awamu ya tano, ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi kwa faida ya
kizazi cha sasa na baadaye.
Kadhalika kwa wale ambao wanajiona kwamba hawawezi kuendana
na kasi hiyo wameshauriwa wajiondoe mapema, kabla mkono wa sheria haujawafikia
ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kuwapata hapo baadaye.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith
Mahenge wakati alipokuwa akizungumza na wakuu wa idara wa halmashauri ya mji wa
Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani humo, katika kikao cha kazi kilichofanyika
mjini hapa.
“Tunataka kazi zote za maendeleo ya wananchi zitekelezwe kwa
wakati, serikali haitaki kuona mtumishi akifanya mambo ambayo hayafanani na
taratibu zake zilizopo”, alisema.
Dkt. Mahenge alieleza kuwa haipendezi kusikia katika
halmashauri kunakuwa na vitendo vya ufisadi na kwamba alimuagiza Mkuu wa wilaya
ya Mbinga, Cosmas Nshenye endapo ataliona hilo linafanyika katika wilaya yake
achukue hatua haraka dhidi ya wahusika ili iweze kuwa fundisho kwa wengine.
Hata hivyo aliongeza kuwa serikali haitaki kusikia mambo
yakienda hovyo badala yake imekuwa ikitaka kuona wananchi wanahudumiwa kwa
misingi, sheria na taratibu zilizowekwa ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo kwa manufaa ya jamii.
No comments:
Post a Comment