Kutoka kulia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Kassim Ntara akisisitiza jambo katika sehemu ya ziara zake za kikazi wilayani humo. |
Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.
JAMII hapa nchini imetakiwa kuhakikisha kwamba watoto wao
wanawapeleka shule na kuhakikisha kwamba wanahudhuria masomo yao kikamilifu,
ukizingatia kwamba elimu ndiyo urithi uliobora maishani mwao na wenye
manufaa makubwa hasa katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia.
Mwenyekiti wa Kamati ya elimu, afya na maji baraza la Madiwani
wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Kassim Ntara alisema
hayo wakati alipokuwa akizungumza na madiwani wenzake wa halmashauri hiyo
katika hafla fupi ya kupokea msaada wa madawati 90 yaliyotolewa na benki
ya CRDB tawi la Songea kwa ajili ya shule za wilaya hiyo.
Ntara alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya ulimwengu wa
sasa ni muhimu kwa wazazi na walezi wilayani humo, wakati wote kuwekeza zaidi
katika elimu kwa watoto wao, badala ya kuwarithisha vitu ambavyo baadaye
vitakuwa tatizo na kuleta mifarakano katika familia zao.
Alisema kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano inayoongozwa
na Dkt. John Magufuli kutangaza mpango wa elimu bure kuanzia darasa la kwanza, hadi
kidato cha nne ni kutaka kuona kila Mtanzania anapata elimu
ambayo itamwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika
maisha yake.
“Madawati haya yamefika kwa muda muafaka ambapo
tuna mahitaji makubwa kwa ajili ya kumaliza upungufu wa madawati kwa shule zetu
za msingi na sekondari hapa Namtumbo, tunawashukuru wenzetu hawa wa CRDB kwa
msaada huu”, alisema Ntara.
Ntara alieleza kuwa pamoja na kupata msaada huo lakini bado
wilaya hiyo inakabliwa na changamoto ya upungufu wa miundombinu ya umeme,
maabara, vyoo, nyumba za walimu madarasa na upungufu mkubwa wa walimu katika baadhi
ya shule za msingi na sekondari.
Kwa upande wake Ofisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Albert
Mbilinyi ambaye pia ni Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ameishukuru
benki hiyo katika kuunga mkono juhudi hizo huku akiwataka wadau wengine kuiga
mfano huo ili kuweza kumaliza tatizo hilo la upungufu madawati wilayani humo.
Mbilinyi aliupongeza pia uongozi wa CRDB kwa kufungua tawi
lake mjini Namtumbo, kwani hatua hiyo inawarahisishia wananchi wa wilaya hiyo
kuweza kupata huduma za kibenki kwa ukaribu zaidi.
No comments:
Post a Comment