Lori hili lenye namba za usajili T 231 BCH ndilo ambalo limesababisha maafa hayo. (Picha na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WATU watatu wakazi wa Tanga pachani kata ya Mbinga mjini
mkoani Ruvuma, wamenusurika kupoteza maisha yao baada ya lori lililokuwa
limebeba shehena ya magunia ya mahindi, kuacha njia na kuparamia nyumba wakati
wakiwa wamekaa ndani ya nyumba hiyo wakipata mlo wa mchana.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa
lilitokea Septemba 8 mwaka huu, majira ya saa 6:32 mchana ambapo lori hilo
lenye namba za usajili T 231 BCH mali ya Mfanya biashara mmoja maarufu mjini
hapa, Medson Ulendo lilikuwa likitokea katika kijiji cha Kilindi kata ya Matiri
wilayani hapa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Festo Sangana ambaye
ndiye mmiliki wa nyumba ambayo lori hilo liliparamia na kubomoa sehemu kubwa ya
kuta za nyumba hiyo alisema kuwa, ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva
kutokana na kuwa katika mwendo kasi ambapo gari lilimshinda kukata kona ndipo
alisababisha ajali hiyo.
Sangana alifafanua kuwa baada ya dereva kusababisha hali hiyo
alitokomea kusikojulikana na kwamba walitoa taarifa kituo kikuu cha Polisi
wilaya ya Mbinga ambapo askari walikwenda huko na kushuhudia uharibifu
uliofanyika.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye alikuwasili katika eneo la
tukio hilo, alishuhudia majeruhi wanne ambao raia wema walijitokeza na
kuwakimbiza katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga ili kuweza
kunusuru maisha yao.
Kadhalika majeruhi hao ambao ni Anna Ndunguru (40), Frank
Ndunguru (30), Shukran Sangana (26) na mtoto mmoja mdogo aliyetajwa kwa jina la
Sabina Komba mwenye umri wa mwaka mmoja, wote wakazi wa Tanga pachani mjini
hapa.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga
Dkt. Robert Elisha alikiri kuwapokea majeruhi hao na kuongeza kuwa watatu kati
ya hao hali zao zinaendelea vizuri na kwamba Anna Ndunguru amepewa rufaa ya
kupelekwa hospitali ya Misheni Peramiho kwa matibabu zaidi kutokana na kuwa na
hali mbaya.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo jeshi hilo linamsaka dereva wa gari
hilo Erick Mbelle mkazi wa Tangi la maji mjini hapa, ambaye anadaiwa kuendesha
huku akiwa amelewa ndio maana alisababisha ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment