Na Padre Baptiste
Mapunda,
Tunapoanza mwaka huu wa 2015 natoa wito wangu kwa viongozi wa dini na waumini kuacha kutetea dhuluma zinazofanywa na serikali ya CCM dhidi ya raia. Viongozi wa dini kuacha kuombea amani wakati serikali inaendelea kupora pesa na rasilimali za wananchi bila aibu wala hofu na kuvunja haki za binadamu, kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya ulinzi.
Nimalize tu kwa kusema kwamba viongozi wa dini lazima mjue na kutambua kwamba Tanzania ya sasa iliyojaa ufisadi, rushwa, uonevu wa kila aina, dhuluma, ujangili, wizi wa mali ya umma, uporaji wa meno ya tembo, utekaji, utesaji, utoboaji macho, ukwapuaji wa kucha kwa koleo, mauaji ya polisi, wizi wa kura, uvunjaji wa haki za binadamu, ubambikizi wa kesi, matusi na kejeli.
NIMEANDIKA mara nyingi sana juu ya wajibu wa viongozi wa
dini katika jamii. Hao ni viongozi wa
dini lakini pia hawawezi kusahau kuwa ni viongozi wa jamii ambao wanaaminiwa na
watu wengi sana.
Viongozi wa dini ni
wadau wakubwa sana katika suala nzima la ujenzi wa demokrasia, hakiza za
binadamu, maendeleo ya nchi, na utawala bora lakini kubwa zaidi viongozi hawa lazima wahamasishe
uhuru wa mawazo pamoja na kuutetea ukweli na haki sawa hasa kwa
wanyonge.
Mimi sitegemei
kiongozi kuwa mwoga wa kusema ukweli pale ambapo serikali inapokosea halafu
viongozi wa dini tunageuka kuwa wanafiki. Hii siyo injili ya Yesu Kristo na
siku zote injili ya Yesu inasema
viongozi wa dini ni “manabii” katika jamii.
Mwaka huu 2015 ni mwaka
wa pekee sana katika nchi yetu kwa sababu ya matukio muhimu hasa ya uchaguzi
mkuu na upitishwaji wa katiba inayopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ninayoiita
katiba “haramu ya CCM.”
Kutokana na masuala
hayo na makando kando yake kama “umuhimu wa kuunda tume huru ya uchaguzi, uandikishwaji na
uboreshwaji wa daftari la wapiga kura, viongozi wa dini wanamezewa mate mengi
sana na wanaccm kuona kama watakuwa upande wao au wa wapinzani, au watabaki katikati
kutafuta maslahi ya jamii.
Kama alivyosema
Mwadhama Cardinali Pengo katika sikukuu ya kusherehekea miaka 70 ya uhai wake
kwamba tulipofikia kama nchi sasa tunahitaji mabadiliko. Alikwenda mbali zaidi nakusema
kwamba mabadiliko haya yataletwa kwa kuunganisha nguvu za watu maskini ili
kuwaondoa viongozi matajiri waliopo madarakani.
Viongozi waliopo madarakani
ni wa CCM ambao wanaunda serikali yenye mamlaka. Na watanzania
tumeshuhudia wizi wa mali wa mabilioni
ya pesa kuanzia Richmond, Epa, Kagoda, Rada na sasa Escrow wizi huo unawahusisha
hasa viongozi wa serikali hii na hili linadhihirishwa
na kufukuzwa kwa mawaziri na watendaji
wengine wa serikali kama vile Mwanasheria mkuu.
Katika hili inaonekana
kama serikali hii ya chama tawala kazi yake kubwa ni kulinda na kutetea wezi wa
mali ya umma. Je, viongozi wa dini hatuelewi hilo au tunajifanya tunaishi
katika dunia nyingine? Kwa mantiki hiyo mimi nashangaa sana ninaposikia makongamano ya kuombea amani
lakini ndani yake mnawachomeka viongozi
wa serikali waje kuzindua, mimi naona hii ni dhihaka kwa Mungu.
Wakati viongozi hao hao wa serikali ndiyo
wanaoharibu amani kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya ulinzi halafu
wanaalikwa kushiriki katika makongamano
ya kuombea amani haingii akilini na rohoni
mwangu. Hii ni kufuru mbele ya mwenyezi Mungu ajuaye yote yaliyo moyoni mwetu.
Tunapoanza mwaka huu wa 2015 natoa wito wangu kwa viongozi wa dini na waumini kuacha kutetea dhuluma zinazofanywa na serikali ya CCM dhidi ya raia. Viongozi wa dini kuacha kuombea amani wakati serikali inaendelea kupora pesa na rasilimali za wananchi bila aibu wala hofu na kuvunja haki za binadamu, kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya ulinzi.
Viongozi wa dini nawashauri acheni kutumiwa na utawala huu wa chama
hiki kuitisha mikesha ya maombi
ambayo hayazai matunda. Tangu mikesha
hiyo ianze na viongozi wa serikali kuhudhuria mbona hakuna mabadiliko? Wizi wa
mali ya umma unaendelea, polisi wanazidi kuua raia hovyo, ukandamizaji, matusi
na kejeli kwa viongozi wa dini, acheni kununuliwa nyie ni viongozi wa dini.
Namna nyingine mimi
napendekeza mikesha hiyo iwe ni fursa ya
kulaani vitendo dhalimu vya serikali ya CCM,
ili watambue kwamba wanachofanya si
kizuri. Viongozi wa dini muwe na ujasiri wa kuikemea serikai hii ili iache
kuendekeza mfumo wa kuendesha serikali kwa manufaa ya chama na siyo wananchi
maskini wa Tanzania.
Viongozi wa dini mna
nafasi nzuri sana ya kukemea maovu ya serikali yanayokiuka haki za binadamu kwa raia wake, Mimi nakumbuka kule Kenya kipindi
cha utawala wa Rais Moi chini ya KANU kulikuwa na unyama mwingi sana
ukiendeshwa na KANU, lakini viongozi wa dini walifunguka wakakemea kwa nguvu na akili zote.
Viongozi wa dini zote
waliungana walipaza sauti zao kama alivyosema Cardinali Pengo kwamba wasiposikia basi mawe yatasikia. Hatimaye waumini wote
nao bila kujali dhehebu wakaungana na wananchi kupitia sanduku la kura wakaiondoa
KANU madarakani na ikazikwa katika
kaburi ka kusahaulika ipumzike kwa Amani
(R.I.P).
Kanisa la Romani kwa
mfano lilimwandikia Rais Moi, barua ya kumwelezea jinsi maovu yaliyokuwa
yanaendeshwa na wakuu wa Wilaya, Mikoa, Usalama wa taifa, Polisi kwa jina lake
bila kumwogopa. Ukweli na uhuru ulitawala mioyoni mwa viongozi wa
dini hapakuwa tena na muda wa kuogopa
kufa.
Viongozi wa madhehebu
mengine walifungwa jela kwa sababu ya kutetea wananchi kama mchungaji Tom Njoya
wa kanisa la Presbyterian. Naye Askofu
wa dhehebu la Anglikan aitwaye Alexander Muge aliiambia serikali ya Moi kwamba “kanisa linawajibu wa
kupinga haki za binadamu zilizotoka kwa
Mungu na uhuru vinapovunjwa na lazima tuwatetee wanyonge wasio na sauti.”
Hii ni mifano michache tu ninayoikumbuka, lakini
ipo mingi kama ya Askofu mkuu mstaafu wa
Jimbo Kuu la Nairobi, Mwananzeiki Ndingi ambaye alikuwa mwiba kwa uongozi wa
KANU.
Mjadala wangu
huu haulengi kujenga chuki na uhasama na
viongozi wa serikali ya Chama cha mapinduzi kama wengi watakavyofikiria, bali
ni wajibu wa viongozi wa dini
kuionyesha serikali kwamba, sasa imefika
mahali imepotoka katika utendaji wake.
Nakumbuka enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere alikuwa
anapenda kukutana na viongozi wa dini na kupata ushauri, kwa kweli alikuwa nao
karibu sana na hivi aliweza kuelewa
walikuwa wanaionaje serikali yake na hivi kujirekebisha.
Lakini serikali ya
awamu ya nne naona imefanikiwa kujiweka mbali na viongozi wa dini na hivi
kuendelea na sera zake za ufisadi, dhuluma, na vitisho kwa wananchi wake bila
kuwa na hofu ya Mungu. Viongozi wa serikali kuongoza nchi bila kuwa na hofu ya
Mungu ni janga na hapo ndipo tulipofikia Tanzania kubaki nchi ya dhuluma na udhalimu kwa wananchi wake.
Kuendelea kuandaa mikesha ya kuombea amani na kuwaalika
viongozi wa serikali kunaijengea kiburi serikali hii ya chama hiki tawala,
kwamba bado inakubalika na kwamba hakuna tatizo lolote nchini kitu ambacho siyo
kweli na hii ni alama ya upofu wa kiuongozi na ulevi wa madaraka.
Lakini kuna wakati
inatupasa kuipa serikali kiashirio kwamba sasa mmepotoka katika utendaji wenu,
hivi nasi tunawaacha kwa sababu
tutakwenda kinyume na injili ya Bwana. Hata Mungu alipobaini mfalme fulani anakiburi
na hasikii basi aliachana naye na huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
Nimalize tu kwa kusema kwamba viongozi wa dini lazima mjue na kutambua kwamba Tanzania ya sasa iliyojaa ufisadi, rushwa, uonevu wa kila aina, dhuluma, ujangili, wizi wa mali ya umma, uporaji wa meno ya tembo, utekaji, utesaji, utoboaji macho, ukwapuaji wa kucha kwa koleo, mauaji ya polisi, wizi wa kura, uvunjaji wa haki za binadamu, ubambikizi wa kesi, matusi na kejeli.
Ili kupambana na
maovu hayo nchi hii inahitaji viongozi
wa dini wenye ujasiri wa kukemea maovu hayo kwa uwazi bila kuogopa. Lazima
ifike mahali viongozi wa dini kama kule Kenya
wawe jasiri kama Yohani mbatizaji aliyekatwa kichwa kwa kukemea uzinzi
wa mfalme Herode.
Maana yake hapa ni pana
hivyo hakuna mageuzi, mabadiliko na
mapinduzi yasiyo na sadaka pengine hata kufa kwajili ya mapinduzi hayo. Viongozi wa dini bila kuchochea chuki, vurugu na maafa kama serikali inavyopenda
kutumia propaganda ya Rwanda ifike mahali tusimame kidete kutetea wananchi
maskini kwa kusema SASA IMETOSHA na
siku hiyo itakuwa mwanzo wa mageuzi.
Ukombozi wa Tanzania
kutoka mikononi mwa CCM unategemea sana mwamko wa viongozi wa dini nchini. Je,
mmeanza kuamka?
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment