Hapa ni Jalalani karibu na shamba la mahindi mtaa wa Kiwandani Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambako watoto sita waliokota kifaa chenye nyaya nyingi, ambacho baadae kiliwalipukia na kuwajeruhi. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
WATOTO wanne kati ya sita wamenusurika kifo, wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma baada ya kuwalipukia kitu ambacho kimeunganishwa na nyaya
nyingi na kuwajeruhi vibaya, wakati mwenzao mmoja akiwa amekishika anaunganisha
nyaya hizo walipokuwa wanacheza pamoja.
Taarifa za awali ambazo zilisambaa mjini hapa, ilielezwa kuwa
mlipuko huo ulitokana na kitu ambacho kilizaniwa kuwa ni bomu ambalo
limetengenezwa kienyeji, jambo ambalo sio kweli.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela, ambaye alikuwa
eneo la tukio alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alithibitisha kuwa, tukio hilo limetokea
leo majira ya saa 5:00 asubuhi katika mtaa wa Kiwandani mjini hapa, wakati watoto hao
wakiwa wanachezea kitu ambacho kilikuwa kimeunganishwa na nyaya nyingi.
Msikhela alikitaja kitu hicho kuwa ni kilipuzi ambacho
hupenda kutumika na watafiti wa madini migodini au walipuaji baruti, huku
akieleza kuwa tukio hilo ni la bahati mbaya ambapo liliwakumba watoto hao baada
ya kuokota kifaa hicho jalalani.
Aliwataja watoto waliolipuliwa kuwa ni Philiberth Mbungu (10),
Augustino Millanzi (5), Geofrey Ndunguru (8) na Emmanuel Mwingira (7) ambao wote
wameumizwa sehemu mbalimbali huku wengine wawili Ayubu Methew (10) na Hassan
Mapangi (5) wakiwa na majeraha ya kawaida mwilini.
Mwandishi wetu ambaye alitembelea katika eneo la Hospitali ya
wilaya ya Mbinga, na kuzungumza na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Elisha
Robert alifafanua kuwa mtoto Philiberth na Augustino wamekimbizwa katika
hospitali ya mkoa Songea kwa matibabu zaidi.
Alisema watoto hao wamepelekwa huko kutokana na kujeruhiwa vibaya
sehemu za usoni machoni, ambapo alieleza kwamba kuna vipande vidogo vidogo vya
vyuma vimeingia ndani yake.
“Niliamua kuchukua hatua ya kuwapeleka hospitali ya mkoa ili
wakapatiwe matibabu zaidi, kutokana na jinsi nilivyowaona hali zao sio nzuri na
mimi nipo kwa karibu sana naendelea kufuatilia kujua hali zao zipoje lakini
taarifa nilizonazo tayari wamepokelewa na wanahudumiwa”, alisema Robert.
Kadhalika aliongeza kuwa Geofrey na Emmanuel wanaendelea
kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, ambapo nao wamejeruhiwa
usoni na mikononi na hali zao zinaendelea vizuri.
Awali Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
alisema uchunguzi unaendelea kufanyika juu ya tukio hilo, na kwamba alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwa waangalifu na watoto wasiwaache wakitembea
hovyo, hivyo pale wanapoona kitu chenye muunganiko wa nyaya wasikiguse badala yake
watoe taarifa haraka kwenye vyombo vya usalama ambavyo vipo karibu nao.
No comments:
Post a Comment