Na Waandishi wetu,
MGOMO wa Wafanyabiashara wa mduka umesambaa mikoa kadhaa hapa
nchini, kupinga matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).
Mgomo huo ulioanzia kwa wafanyabiashara wa maduka Kariakoo Jijini
Dar es Salaam kuanzia juzi, kupinga Mwenyekiti wao Johnson Minja, kukamatwa na
polisi, sasa umesambaa hadi miji ya Mwanza, Iringa, Songea na Dodoma.
APANDISHWA KIZIMBANI:
Minja (34) jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili, likiwamo la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa
kutumia EFDs na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Rebbeka Mbiru.
Wakili wa Serikali, Godfrey Wambari alidai kuwa Septemba 6
mwaka 2014 katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango Dodoma alitenda kosa la kushawishi
wafanyabiashara, kutenda kosa la jinai kwamba wasilipe kodi.
Katika shitaka la pili, siku na mahali pa tukio la kwanza
mshtakiwa anadaiwa kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za EFD. Upande
wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana.
Mshtakiwa alikana mashitaka yake;
Hakimu Mbiru alisema mshtakiwa huyo, atakuwa nje kwa dhamana
kwa kuwa na wadhamini wawili akiwemo mtumishi wa serikali mmoja, watakaosaini
hati ya dhamana ya shilingi milioni nne.
Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga alidai kuwa mshtakiwa ni
mfanyabiashara maarufu nchini na kwamba anaaminika hawezi kutoroka, hivyo
mahakama ipunguze masharti ya dhamana.
Hata hivyo, mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi
hiyo itatajwa Februari 11, mwaka huu.
IRINGA:
Katika hatua nyingine, wakazi wa mkoa wa Iringa nao
walishindwa kupata huduma muhimu kutokana na wafanyabiashara wenye maduka
kuungana na wafanyabiashara wa mikoa mingine, katika mgomo wa kufungua maduka
baada ya Minja kukamatwa.
Mgomo huo umedumu kwa siku nzima, na kusababisha wakazi wa Manispaa
ya hiyo kukosa huduma muhimu za kijamii.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Iringa, Odilo Nambanga
alisema kwamba mgomo huo wameungana na wenzao nchi nzima, kufunga biashara zao
mpaka matatizo yao ya msingi yatakapotatuliwa.
Nambanga alisema kauli mbiu yao ni Mwenyekiti kwanza, na
masuala mengine yatafuata ikiwa ni pamoja na kuungana kwa umoja wao na kutatua
matatizo yao.
Naye mfanyabiashara Sylivester Mmasi, alisema hawawezi
kufungua biashara hata zipite wiki mbili hadi watakapopata tamko la kukamatwa,
mwenyekiti wao.
Alisema umesababisha wanafunzi kukosa huduma za vifaa vya
shule, hasa wale wanaokwenda shule zilizopo nje ya Manispaa ya Iringa, na
kulazimika kushindwa kuhudhuria masomo.
SONGEA:
Kadhalika wafanyabiashara wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
wamelazimika kufunga maduka yao kupinga kitendo cha kukamatwa kwa Minja na
kwamba mgomo huo utadumu mpaka hapo, watakapopata uhakika wa usalama wake na si
vinginevyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo
tawi la Ruvuma, Isaya Mwilamba alisema wamefunga maduka kusubiri hatma ya
Minja.
Mwilamba alisema kuwa wafanyabiashara wote nchini,
wanasitisha shughuli zote hadi watakapojua hatma ya kiongozi na mtetezi wao.
“Tunaitaka serikali kuzingatia nia njema ya kuundwa kwa
kamati hiyo ya majadiliano, na itoe taarifa stahiki kwa wafanyabiashara kwani
tunapata wasiwasi kuwa kukamatwa kwake kiongozi wetu, kunatokana na juhudi za
wafanyabiashara kupinga ongezeko la kodi kwa asilimia 100 na matumizi ya
mashine za EFD,” alisema Mwilamba.
Alisema serikali inapaswa kutumia njia za kidemokrasia
kumaliza changamoto zake na siyo kutumia nguvu kuzima madai ya msingi ya
wafanyabiashara, hivyo ni vyema ikasikiliza kilio cha wafanyabiashara ambao
kimsingi ndio wachangiaji wakubwa wa kodi za serikali.
MWANZA:
Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka jijini Mwanza wa mitaa ya
Lumumba, Pamba na Rwegosore, wamefunga maduka kupinga kukamatwa kwa Minja.
Michael Massanja, mfanyabiashara wa jijini hapa alisema
wamesikitishwa kukamatwa kwa kiongozi wao na wameamua kuungana kwa kufunga
maduka, kama walivyofanya wenzao wa Dar es Salaam.
Massanja alisema kukamatwa kwa kiongozi wao sio suluhisho la
kuwafanya wafanyabiashara kutumia mashine hizo, badala yake serikali izungumze
na wafanyabiashara husika ili kutatua mgogoro huu uliopo.
”Hatutafungua maduka yetu hadi pale tutakapopata taarifa ya
Mwenyekiti wetu mahali alipo ingawa tumesikia yupo Dodoma, lakini hatuna
uhakika na hilo,” alisema Massanja.
Naye Zuberi Issa, mfanyabiashara wa maduka mtaa wa Pamba,
alisema kufuatia kukamatwa kwa Mwenyekiti wao Minja, kumesababisha kutofanyika
biashara yoyote kwa siku nzima ya jana, huku akisisitiza maduka kutofunguliwa.
”Tukio hili limechangia tusifanye biashara toka asubuhi kwa
kuwa tumesisitiziwa na wenzetu kuungana ili tujue hatma ya kiongozi wetu yupo
wapi na atapatikana lini,” alisema Issa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza,
Christopher Wambura, hakupatikana kuzungumzia mgomo huo.
KARIAKOO BADO:
Wafanyabiashara wa Soko Kuu Kariakoo Mtaa wa Kongo, jijini
Dar es Salaam, wameendelea kugoma kufunga maduka yao kushinikiza kuachiwa kwa
Minja.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE ulibaini kuwa karibu
mitaa yote inayopatikana Karikoo, maduka mengi yalikuwa yamefungwa jana huku
machache yakiwa yamefunguliwa.
Katika Mtaa wa Kongo, wafanyabiashara walikutwa wakiwa nje,
hali iliyowawia vigumu wateja kupata mahitaji kama vile bidhaa kadhaa.
NIPASHE lilibaini baadhi ya maduka ya simu machache
yaliyokuwa yamefunguliwa milango nusu hali iliyowafanya wateja kununua bidhaa
za hizo kwa taabu.
Walipohojiwa wafanyabiashara hao kwa masharti ya kutotajwa
majina yao, walisema wataendelea kugoma kufungua maduka yao hadi watakapojua
sababu ya kukamatwa kwa kiongozi wao.
“ Hatufungui maduka yetu mpaka tujue sababu ya kukamatwa kwa
Minja, tutayafungua endapo tutaelezwa sababu za kukamatwa kwake,” alisema mmoja
wa wafanyabiashara hao.
Minja alikamatwa juzi na Jeshi la Polisi na
kusafirishwa kupelekwa mjini Dodoma kujibu mashitaka ya kuhamasisha
wafanyabiashara wa mkoa huo wagome kufungua maduka kupinga matumizi ya EFDs.
Imeandikwa na Daniel Mkate, Mwanza, Peter
Mkwavila, Dodoma; Gideon Mwakanosya, Songea; George Tarimo, Iringa na Hussein
Ndubikole, Dar.
CHANZO: NIPASHE.
No comments:
Post a Comment