Monday, January 19, 2015

WASIMAMIZI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA MBINGA WAENDELEA KULALAMIKIA KUPUNJWA MALIPO YAO, WAMTAKA WAZIRI MWENYE DHAMANA KUINGILIA KATI


Hawa Ghasia, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI.
Na Mwandishi wetu,

TUMEKUWA tukijiuliza maswali mengi lakini majibu hatuna, kubwa zaidi juu ya hatma yetu kama wafanyakazi ndani ya Halmashauri ya wilaya yetu ya Mbinga hapa mkoani Ruvuma, licha ya kuishi katika mazingira magumu baadhi yetu tumekuwa wafanyakazi tusiosikilizwa, tunaobezwa, kuzarauliwa, hata hatupaswi kuhoji wala kudai na kutimiziwa haki zetu za msingi.

Katika hali ya kawaida utumishi au kufanya kazi katika wilaya hii naweza nikasema imekuwa ni kero na mtihani mgumu mithili ya Swala ndani ya ngome ya Simba na Chui au utumwa katika nchi yao.

Tunajiuliza haya yote yanafanyika yanabaraka kutoka wapi? hivi jee Mkurugenzi wa wilaya hii, Hussein Ngaga ambaye ndiye mwajiri wetu anajua au kutambua thamani ya utumishi wa umma? au uongozi katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga imekuwa kama jambo la mzaha lisilohitaji busara weledi na taaluma,……………wakati wote tumekuwa tukijiuliza maswali haya kwa mwenendo uliopo sasa tunabaki kuumia kichwa tu.

Tulitaraji uongozi wa halmashauri ukiongozwa na mkurugenzi akiwa ndiye mwajiri, uwe makini katika kushughulikia matatizo ya watumishi wenzake lakini cha ajabu amekuwa kimya na chanzo cha kubeza kero na changamoto za watumishi wake, zaidi kumekuwa na manyanyaso yanayochangiwa na ofisi yake hasa kwa kupuuza haki stahiki za wafanyakazi.


Kwa mfano hivi karibuni wakati zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa lilipokuwa likifanyika, tumeshuhudia malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi hasa wale walioteuliwa kusimamia zoezi la uchaguzi huo kwa ngazi ya chini na licha ya malalamiko hayo nguvu kubwa ilitumika ikiwa ni pamoja na usiri wa taarifa, hususani hata malipo sahihi kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo.

Walioonyesha nia yakuhoji malipo sahihi walijibiwa majibu yasiyo ya kuridhisha ikiwa ni pamoja na kauli za subiri cheki haijasainiwa? muda ukifika mtapata? wenzio hawahoji wewe ni nani? nasisi hatujui? yote haya yalikuwa na siri kubwa licha ya walioteuliwa kufanya kazi hiyo bila kinyongo na hatimaye uchaguzi ukaisha salama, lakini tatizo likawa ni stahiki gani wanatakiwa kulipwa hapo ndipo kikawa kitendawili na kuwaacha wafanyakazi wengi walioshiriki katika zoezi hilo kuwa njia panda?

Katika mazingira ya woga wengi wao walikubaliana na malipo yaliyotolewa licha ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo kutoridhika na malipo ambayo hayaendani na hali halisi ya maisha, ugumu na pia waraka husika wa malipo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliotolewa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwa kwa wasimamizi wasaidizi wanapaswa kulipwa shilingi 105,000 na sio 50,000 kama walivyolipwa katika wilaya ya Mbinga.

Kwa mchanganuo ilikuwa kila msimamizi alipwe shilingi 10,000 kwa kila siku, kwa siku saba za kuandikisha wapiga kura na sio shilingi 5,000 kama walivyolipwa na shilingi 35,000 siku ya uchaguzi inayojumuisha siku ya maandalizi pamoja na kuchukua vifaa vya uchaguzi, siku ya uchaguzi na kukabidhi vifaa na sio shilingi 15,000 kama walivyolipwa.

Licha ya malipo kutokuwa sahihi hatujaona jitihada zozote zile kutoka kwa viongozi wa halmashauri yetu, inayokusudia kutimiza haja na matakwa ya wafanyakazi wote walioshiriki kusimamia zoezi la uchaguzi huo, tumeona tu tukidharauliwa na kukejeliwa kwa lugha mbovu ikiwa ni mvuta bangi, mlevi kwa sababu tu amehoji haki yake na zaidi kutishiwa usalama wa ajira yake.

Ukimya kutoka ofisi ya Mkuu wa wilaya, Mkurugenzi na Mbunge unatupa wasiwasi ni kitu gani kimejificha ndani yake juu ya sisi tuliofanya kazi hii tusipate haki zetu za msingi ipasavyo, na jee ipi ni hatma yetu kuhusiana na malipo sahihi licha ya ofisi zote kuwa na taarifa sahihi ya mapunjo kwa wafanyakazi waliosimamia zoezi hili la uchaguzi wa serikali za mitaa hapa Mbinga.

Jee watumishi tutarajie nini kudhulumiwa, kusahau, kulipwa au tuishie kutishwa, kukejeliwa, kutukanwa kama ndio njia muafaka ya kutatua madai yetu kwa mwajiri juu ya mapunjo yaliyofanyika katika malipo ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014.

Hivi tujifunze nini kutoka kwenu ambapo serikali iliwaamini kuja kuongoza wanakondoo hawa wa Mbinga, na leo hii mnaonyesha uaminifu mdogo hasa kwa jambo hili. Je katika chaguzi zijazo kabla ya malipo tupokee rushwa kutoka kwa wagombea au vyama vya siasa ili kufidia mapunjo ambayo tunaweza kukutana nayo.? Hivi viongozi ndani ya halmashauri yetu wanachukuliaje dhana ya uongozi au wanaona ni jambo la mzaha lisilohitaji kutiliwa mkazo?..............yatupasa tubadilike katika hili.

Tunashindwa kuelewa kama viongozi wetu wana nia njema yakupambana na rushwa hasa kipindi hiki cha uchaguzi kwani kwa kutowapa stahiki zao wale waliofanya kazi mnatufundisha nini, hivyo tunashindwa kujua uadilifu na dhamira ya viongozi wetu wa Mbinga hasa kwa mkurugenzi mtendaji ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia zoezi zima la uchaguzi?.

Tumekatishwa tamaa na jinsi mkurugenzi Ngaga anavyoshughulikia kero, matatizo na changamoto za wafanyakazi wake hivyo, hatma yetu tunaiona ipo rehani maana yake amekuwa ni mtu wa kupuuza mambo.

Pia tunaamini dhuluma imetendeka dhidi yetu kwa kuwa haiwezekani kazi ile ile na ugumu ule ule mtu aliyefanya kule Morogoro, hata kwa ndugu zetu walio jirani wilaya ya Nyasa walipwe vizuri na aliyepo Mbinga apunjwe, hakika hii ni dhuluma na ubaguzi ambao haupaswi kuungwa mkono.

Tutaendelea kulaani dhuluma hii na ubaguzi huu kwa kumtaka Waziri mwenye dhamana awajibike au amwajibishe mkurugenzi huyu wa Mbinga, ili iwe fundisho kwa wengine kwa kutotambua wajibu wake kama kiongozi aliyelishwa kiapo na kuwekwa madarakani kuwatumikia wananchi ipasavyo, ili ajue uongozi ni jambo linalohitaji busara ya hali ya juu na sio mzaha.



No comments: