Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KUCHELEWA kunyesha kwa mvua katika maeneo mbalimbali mkoani
Ruvuma, kumesababisha wakulima kupatwa na wasiwasi juu ya hali ya uzalishaji wa
mazao ya chakula na biashara, katika msimu huu wa kilimo hasa ikizingatiwa kuwa
misimu iliyopita mvua ilikuwa ikianza kunyesha mkoani humo katika mwezi Novemba
tofauti na ilivyo sasa.
Katika maelezo yao kwa waandishi wa habari kwa nyakati
tofauti, wakulima wa wilaya za Namtumbo na Songea mkoani humo walisema, hali
hiyo ya mvua kuchelewa kunyesha imeshaanza kuwatia hofu kubwa kwani tayari
walishafanya maandalizi yote ya kilimo, ikiwemo kupanda mazao mashambani lakini
hadi sasa mvua imekuwa ikinyesha kwa kusuasua.
Walisema hadi sasa mazao waliyopanda yameanza kuota lakini
yanakauka kutokana na kukosekana kwa mvua za kutosha na kwamba hata wadudu
wamekuwa wakijitokeza na kushambulia mimea iliyoota.
“Mwakani tuna wasiwasi sana juu ya hali ya chakula katika
mkoa huu, kwani mvua ambazo tunazitegemea kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi
Novemba mvua zimekuwa zikinyesha kwa suasua, na mazao yanakauka shambani
kutokana na kukosa maji ya kutosha”, walisema.
Naye Damas Hyera mkulima wa kijiji cha Liganga wilaya ya
Songea alisema, upungufu huu wa mvua ulioanza kujionyesha sasa katika
maeneo mbalimbali ni ishara tosha ya wananchi kujiwekea akiba ya chakula kwani
inawezekana kukatokea baa kubwa la njaa katika msimu huu wa 2015 – 2016
na kwamba ni vyema serikali ikaanza kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na
hali hiyo.
Naye Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akifafanua juu ya
hali hiyo aliwataka wakulima wa mkoa huo kuzalisha mazao yanayostahimili ukame
kama vile mhogo, na kwamba aliwaaagiza maafisa kilimo kuacha kukaa maofisini
badala yake wapiti vijijini na kutoa elimu kwa wakulima kuhusiana na uzalishaji
wa mazao hayo ambayo yanastahimili ukame.
Mwambungu aliongeza kuwa kila kaya inapaswa kujenga tabia ya
kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha, kulingana idadi ya familia ili kuepuka
uwezekano wa kupatwa na njaa jambo ambalo ni nadra kujitokeza katika mkoa huo.
No comments:
Post a Comment