Padre Baptiste Mapunda. |
Na Padre Baptiste Mapunda,
MIMI siyo nabii lakini leo hii napenda kutoa maono yangu juu
ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huenda kutakuwa na uwezekano wa kumwagika
damu kutokana na usomaji wa alama za nyakati. Tukubali kwamba dunia ya
leo inaogopa sana maono hasa yanayotishia madaraka ya wanasiasa wetu mufilisi.
Maono ni elimu inamhusu Mwenyezi Mungu awezaye na
ajuaye yote, hivyo basi mwanadamu kujidai anajua sawa na Mungu ni kufuru ya
hali ya juu. Lakini Mungu huyo aliyemuumba mwanadamu kwa mfano na sura
yake anaweza kumfunulia mambo fulani ili aweze kuwaeleza wanadamu kuwaonya,
kuwahabarisha au kuwaelekeza.
Maovu yanavyoendelea kutokea katika nchi yetu kwa
kusoma alama za nyakati najiuliza swali moja; Je Tanzania
inakwenda kuingia katika historia ya umwagaji damu uchaguzi mkuu wa mwaka
huu? Hakika kwa maovu mengi ya nchi yetu sasa hivi ni wazi nchi haipo salama.
Nchi yetu kwa muda wa miaka mitatu sasa imepitia
katika matukio na maovu ya ajabu ambayo yanashitua mustakabali wa
jamii mzima, kumekuwa na mauaji ya Albino, na utekaji wa raia
wema na kujeruhi mfano Dokta Ulimboka, marehemu Dokta Mvungi, yakiwemo mauaji
ya mwandishi wa habari David Mwangosi.
Taifa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaendelea
kutikiswa na ufisadi wa mabilioni ya pesa za wananchi, bila hatua maalumu
kuchukuliwa.
Uvunjaji wa haki za binadamu umeendelea kutokea mara
kwa mara, usalama wa raia umetikiswa mara nyingi na leo tunashuhudhia “Panya
road” wakihatarisha maisha ya raia Jijini Dar es salaam, bila jeshi la polisi
kuwa na uhakika Panya road ni nani hasa?
Utekaji, ukandamizaji wa vyama vya upinzani, kujeruhi na hata
kuua wanachama wao katika mikutano umeendelea kutokea na serikali
kushindwa kuchukua hatua kwa wauaji hao.
Udini umeingizwa katika siasa na umewagawa waumini wa
madhehebu mbalimbali kwa kupandikiza chuki.
Kulipua Parokia ya Olasiti Arusha, mbele ya mwakilishi
wa Baba Mtakatifu na kupelekea watu watatu kufa na makumi kujeruhiwa, ni alama
mbaya sana ya kuelekea umwagaji damu katika nchi yetu.
Wizi wa mabilioni ya pesa EPA, Richmond, Kagoda, na sasa
Escrow ni alama ya kukosekana kwa amani. Kwa matukio niliyoonyesha hapa ni wazi
Tanzania sasa inaelekea kumwaga damu hasa katika kipindi cha
uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015.
Nasema sasa kwa uwazi na uhuru ili serikali ya CCM isipate
kisingizio kwamba haikujua, sasa inajua kwamba kinachoendelea ni maandalizi ya
vurugu, maasi, chuki, fitina na maafa kwa wananchi.
Uchaguzi wa serikali za mitaa ni alama tosha ya umwagaji damu
ninayozungumzia katika makala haya, uchaguzi huo haukuandaliwa vizuri na
mwishowe ni kuibeba ccm kwa mabavu na mabomu. Je huku si kuandaa maafa wakati
wananchi wanajua umuhimu wa kupiga kura yao?
Matokeo yake uchaguzi uligubikwa na kasoro
lukuki, fitina, mizengwe, upendeleo, ubaguzi, vitisho, kujeruhiwa na hata
wengine kuuawa. Je hii ndiyo amani inayohubiriwa na ccm kila kukicha?
Pamoja na maeneo mengine chama hiki cha mapinduzi
kushindwa, lakini ubabe bado unaendelea kuonyeshwa kwa kuwatangaza
wanaccm walioshindwa na hata kulazimisha waapaishwe. Je nani anahatarisha
amani ya nchi wapinzani au wanaccm? Na sisi viongozi wa dini tuhubiri
amani ipi sasa?
Sasa hivi wanatengeneza machafuko kupitia uchaguzi mkuu
utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. CCM lazima wajue kwamba gharama ya
uchakachuaji wa kura ni machafuko, vita na maafa kama yalivyotokea nchini Kenya
katika ushindi uliochakachuliwa na tume ya marehemu Kivuitu mwaka 2007.
Uchakachuaji huo ulisabaisha wananchi kuyakataa matokeo
ya ushindi huo. Serikali yetu inatupeleka wapi?
Ni vema tutafakari kwani enzi hii ni tofauti na miaka ya
2000, 2005, na hata 2010 wananchi wamebadilika. Sasa hivi Watanzania wameamka
wanataka mabadiliko kama alivyoasa Mwadhama Kardinali Pengo, kwamba
Tanzania ilipofikia sasa inahitaji mabadiliko ambayo yataletwa na watu
maskini kwa kuungana ilikuwang’oa viongozi mafisadi. CCM lazima
ijue sasa mabadiliko hayaepukiki kamwe.
Lazima watambue kwamba enzi ya kuamini kwamba ndiyo chama
pekee na kwamba bila ccm Tanzania haiwezekani zimeisha sasa. CCM imelewa
madaraka, ccm imetekwa nyara na mafisadi kama alivyoasa Mwadhama
Kardinali Pengo katika sherehe ya kuzaliwa kwake.
Uchaguzi mkuu wa mwaka huu ccm watajaribu kutumia kila mbinu
ili kuendelea kubaki madarakani. Watatumia pesa kununua kura, watatupatia
khanga, kofia, pilau, kuahidi vyeo, watatumia wanahabari, watatumia viongozi wa
dini na udini, lakini haitasaidia kitu.
CCM watatumia vyombo vya dola vikiwamo vya ulinzi na usalama,
polisi, FFU, Usalama wa taifa na hata Jeshi la wananchi, lakini havitasaidia,
kwa sababu muda wa mabadiliko umefika.
Wapinzani watauawa na wapenda mabadiliko na maendeleo ya
nchi, watu watabambikizwa kesi hasa wapinzani, kura zitaibiwa, matokeo
yatabadilishwa, na walioshindwa watatangazwa washindi lakini yote hayo
hayataiokoa kutoka katika kaburi la kifo.
Kitakachoikoa chama cha mapinduzi ni kukubali matokeo, na
kuanzia sasa ni kuunda tume huru ya uchaguzi, kuboresha daftari la wapiga kura,
kurekebisha sheria na kanuni mbovu za uchaguzi na kuwa na wasimamizi
watenda haki kwa wote.
Nawaomba viongozi wa dini wasaidie kuiepushe nchi ili
isitumbukie katika machafuko, vita na hatimaye mauaji kama yalivyotokea nchini
Kenya mwaka 2007. Maono yangu yanatokana na kusoma alama za nyakati
ni kwamba serikali ya ccm isipoangalia itaiingiza nchi katika
umwagaji wa damu kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe;
frmapunda91@gmail.com
No comments:
Post a Comment