Na Dustan Ndunguru,
Songea.
WAHITIMU wa mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) nchini,
wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kudumisha amani tuliyonayo
badala ya wao kuwa chanzo cha vurugu hususani, katika kipindi hiki ambapo taifa
lipo katika mchakato wa kupata katiba mpya.
Naibu Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Jenista Mhagama alitoa
rai hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakatialipokuwa akifunga mafunzo ya miezi
mitatu ya kijeshi kwa wahitimu 985 wa kozi ya ualimu
Operesheni miaka 50 ya Muungano, kwa mujibu wa sheria awamu ya pili
mwaka 2014 katika kikosi cha 842 KJ Mlale JKT wilaya ya Songea mkoani
Ruvuma.
Alisema serikali haikukosea kurudisha mafunzo ya JKT kwa
vijana wanaomaliza vyuo, kwani dhamira yake kubwa ni kutaka kuwaandaa na
kuwajenga vijana hao kuwa viongozi bora, na wenye ari kubwa na moyo wenye
uzalendo kwa nchi yao.
Jenista pia aliwataka kukataa kutumika vibaya na watu wenye
nia mbaya katika nchi, kwa kuwatumia kama ngazi ya wao kufanikisha mambo yao
binafsi jambo ambalo litaweza kuhatarisha amani na utulivu uliodumu tangu nchi
ipate uhuru mwaka 1961.
Serikali bado itaendelea kuwaandaa vijana kutoka maeneo
mbalimbali hapa nchini, wanaomaliza elimu ya juu katika vyuo vikuu na vikosi
vya jeshi, ili kuwa viongozi waadilifu watakaokuja kuwaongoza wengine kwa
kuzingatia maadili mema ambayo hayatazua malalmiko kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo alifafanua kuwa, lengo lingine la
mafunzo hayo ya JKT ni kumfanya kijana aweze kujitambua na kutambua majukumu yake
ya kila siku katika maisha yake, na kulitumikia taifa badala ya kuwa
kijana anayetumia muda wake mwingi kukaa kijiweni bila shughuli yoyote na
kuanza kulalamika huku kukiwa na fursa nyingi za kiuchumi.
“Kwa kukosa uzalendo ndiyo maana baadhi ya vijana wengi
nchini hasa wale waliopata nafasi ya kuchaguliwa kufanya kazi katika
maeneo ya vijijini, wengi wao wamekataa kwenda huko kwa kukosa
uzalendo hivyo serikali haitarajii tena kuona wahitimu wanaotoka
katika vikosi vya jeshi la kujenga taifa, wanakuwa na tabia kama hii ya
kushindwa kutumikia watanzania wenzao”, alisema.
Kadhalika aliwasihi wahitimu hao mara watakapofika katika vituo
vyao vya kazi kuwa na moyo wa huruma kwa wanafunzi, pamoja na jamii
itakayowazunguka huku wakikumbuka kuwa serikali imetumia gharama
kubwa wakati wote wa mafunzo yao ya kijeshi, hivyo ni lazima waonyeshe
uzalendo katika kulitumikia taifa lao.
Awali wahitimu hao kupitia risala yao iliyosomwa na
Julieth Soza, walisema kutokana na umoja na ushirikiano mzuri baina ya vijana, wakufunzi
na viongozi kwa ujumla wamepata mafanikio katika sekta ya ujanja wa
porini, matumizi ya silaha na ramani, utimamu wa mwili, sheria za kijeshi,
usalama na utambuzi wa usalama wa ndani, mafanikio mengine ni kuchimba mahandaki,
uokoaji, elimu ya ukimwi, kupiga shabaha, kwata, uraia, uzalishaji mali,
michezo na mbinu za kivita.
Naye mwakilishi Mkuu wa Jeshi la kujenga taifa ambaye pia ni
Mkuu wa utumishi katika jeshi hilo, Kanal Thomas Mbele aliwapongeza
wahitimu hao kwa kuonyesha uvumilivu katika muda wote waliokuwa katika mafunzo
hayo na kwamba jeshi hilo linatambua kuwa vijana hao wanakabiliwa na changamoto
nyingi wanapokuwa mafunzoni.
No comments:
Post a Comment