Dokta Harrison Mwakyembe. |
Na
Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI
wa uchukuzi Dokta Harrison Mwakyembe amesema, serikali nchini imedhamiria
kujenga reli kuanzia Mtwara hadi Mbamba Bay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, jambo
ambalo litarahisisha kazi ya ubebaji wa mizigo mizito ya makaa ya mawe na chuma
kutoka Liganga wilayani Ludewa mkoa wa Njombe.
Akizungumza
na Wadau wa usafirishaji jana katika ukumbi wa Ikulu ndogo mjini hapa, Dokta Mwakyembe
alisema ujenzi wa reli hiyo unatarajiwa kuanza mapema mwakani na kwamba utakamilika
mwaka 2018.
Alisema
kujengwa kwa reli hiyo kutasaidia barabara za lami zilizopo na zinazoendelea
kujengwa katika mikoa ya kusini, kutoharibika mapema kutokana na kupitisha
magari yanayobeba mizigo ya makaa ya mawe na chuma na kuzifanya zidumu kwa muda
mrefu.
“Kujengwa
kwa reli hii kutoka Mtwara hadi Mbamba bay kutakuwa na vituo saba na ujenzi huu
utagharimu shilingi bilioni 3.5 hadi kukamilika kwake, lakini kukamilika huko kutasaidia
sana kuzifanya barabara zetu zidumu kwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba,
ile mizigo ya makaa ya mawe na chuma toka Liganga yatasafirishwa kwa njia ya
reli”, alisema Dokta Mwakyembe.
Kuhusu
ujenzi wa meli mpya itakayosaidia kurahisisha usafirishaji wa abiria katika
ziwa Nyasa, alisema mkataba wa ujenzi unatarajiwa kusainiwa mwezi huu na kwamba
baada ya hapo kazi ya ujenzi wa meli hiyo utaanza mara moja, ambapo kukamilika
kwake kutasaidia pia kuwaondolea adha ya usafiri wananchi.
Pamoja
na kujengwa kwa meli hiyo, mpango uliopo ni kuboresha bandari ya Itungi na
Ndumbi ambapo mpaka sasa mamlaka ya bandari imetenga kiasi cha shilingi milioni
500, kwa ajili ya ujenzi wa ghati katika bandari ya Ndumbi.
Katika
hatua nyingine Dokta Mwakyembe alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanja cha
ndege mjini Songea, alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili
kuhakikisha kuwa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini, inaendelea kuboreshwa
na kuweza kutoa huduma za kuridhisha kwa wananchi.
Alisema
Mamlaka ya viwanja vya ndege ilifanya mazungumzo na benki ya dunia ili kutumia
fedha zilizosalia katika mkopo uliowezesha ukarabati na upanuzi wa viwanja vya
Kigoma, Tabora na Bukoba, kutekeleza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina
katika viwanja kumi na moja ambavyo ni Songea, Iringa, Lake Manyara, Musoma, Tanga,
Kilwa Masoko, Lindi, Moshi, Njombe, Singida na ujenzi wa kiwanja kipya cha
ndege mkoani Simiyu.
“Katika
bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 serikali kupitia mamlaka ya viwanja vya
ndege, tumetenga shilingi milioni 660 za kitanzania toka fedha za ndani na
shilingi milioni 3,200 fedha za kigeni kutoka benki ya dunia, kwa ajili ya
mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja kumi na moja”, alisema.
Hata
hivyo Waziri huyo aliwataka wananchi waliovamia eneo la uwanja wa ndege Songea
na kujenga makazi ya kudumu, waondoke mara moja kwenye maeneo hayo na kwamba
hakuna fidia yoyote itakayotolewa kutokana na hilo.
No comments:
Post a Comment