Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake alivyoketi hapa mkoani Ruvuma. |
Mbinga.
KATIKA hali ya kushangaza, hoja ambayo inadaiwa kupelekwa kwa
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein
Ngaga juu ya kutaka kuvunjwa kwa Kamati ya mipango na fedha ya halmashauri
hiyo, imelalamikiwa na baadhi ya Madiwani wa wilaya hiyo na kuelezwa kuwa ni
batili. Mtandao huu umeambiwa.
Ngaga anashutumiwa na madiwani wake kwamba, mpango huo wa kutaka
kuvunja kamati hiyo amekuwa akiufanya chini kwa chini na tayari suala hilo,
limefikishwa mezani kwake kwa utekelezaji, katika kikao cha baraza la madiwani
kinachotarajiwa kuketi Januari 23 mwaka huu, wilayani humo.
Mpango huo umeelezwa kuwa unajidhihirisha pale mkurugenzi
huyo alipovunja ratiba za vikao vya kamati husika, ambapo hata baraza hilo ilibidi
liketi mwishoni mwa mwezi huu na sio tarehe hiyo, ambapo madiwani wake wameshangazwa
na hali hiyo.
“Ratiba ya vikao vyote vya kamati amevivuruga na kupanga
tarehe anazozitaka yeye, hata baraza hili la madiwani anataka kulifanya mapema
kwa lengo la kuwakusanya baadhi ya watu wake (madiwani) ili waweze kufanikiwa
mipango yao waliyojiwekea”, walisema.
Malalamiko hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na
kufafanuliwa kuwa hakuna kikao ambacho madiwani hao walikaa na kukubaliana
kuvunja kwa kamati hiyo, ambayo ndio mhimili wa kamati zote za baraza la
madiwani.
Walisema kitendo hicho kinachofanywa, ni mpango mchafu ambao
Mkurugenzi huyo wanamtuhumu huenda amekaa na kundi lake la watu wachache, wakiwemo
baadhi ya madiwani na vigogo wa halmashauri hiyo (majina tunayo) ikiwa ni lengo
la kutimiza matakwa yake binafsi.
Aidha inadaiwa kuwa tendo hilo linalotaka kufanyika linatokana
pia na wajumbe wachache waliomo ndani ya kamati hiyo ya mipango na fedha, kuwa
mwiba kwake na kutotaka kuburuzwa wakati wa kupitisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo
ya wilaya hiyo, kinyume na taratibu husika.
“Leo anapotaka kuvunja
kamati hii maana yake ikishavunjwa, kamati zote tulizonazo ndani ya baraza hili
itabidi ziundwe nyingine upya, sisi tunashangaa sana hatuja kaa kikao chochote
kama madiwani na kukubaliana kupitisha maamuzi haya”, walisema.
Kadhalika waliongeza kuwa kuvunjwa kwa kamati hiyo, huenda
kanuni husika za baraza la madiwani hazitaruhusu kufanya hivyo kutokana na kile
walichoeleza kuwa baraza hilo linaelekea mwishoni kuvunjwa, tayari kuelekea
uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu wa kumchagua Rais, Wabunge
na Madiwani.
Hali hiyo imefafanuliwa kuwa ni vyema Mkurugenzi wa halmashauri
ya Mbinga, Ngaga awemakini katika hili azingatie kanuni husika, na endapo kama
zinamruhusu kufanya hivyo kabla ya yote ni muhimu akashirikisha kwanza madiwani
wake, kupitia vikao halali kabla ya kuleta maamuzi katika kikao cha baraza la
madiwani.
Alipotafutwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo,
Ngaga simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa na imekuwa ni
tabia yake ya kutopokea simu, na kukataa kuhojiwa au kuzungumza na waandishi wa
habari hasa pale panapokuwa na malalamiko dhidi yake.
Pamoja na mambo mengine mwandishi wa habari hizi alipozungumza
na Katibu wa Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo, Adolph Mandele
alikiri kuwepo kwa mpango wa kuvunjwa kwa kamati hiyo ya mipango na fedha, huku
akifafanua kuwa mchakato wa kutekeleza hilo unatokana na baadhi ya madiwani kuwa
na tabia ya kuvujisha siri za vikao vya kamati pale vinapoketi.
Mandele alipoelezwa kwamba madiwani wenzake wanashangaa juu
ya maamuzi hayo kuwa hawajashirikishwa na kubariki katika kikao husika, alikana
na kusema kuwa tayari madiwani 28 walihudhuria katika kikao cha chama ambacho
kiliketi kwa dharula Desemba Mosi mwaka jana, na kukubaliana kufanya hivyo.
Katibu huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Mpapa na Katibu
mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo alisema, “suala hili mimi tayari
nimelifikisha kwa mkurugenzi mtendaji kwa maamuzi zaidi, nimemtaka azingatie
kanuni husika za baraza ambazo zitamruhusu kufanya hivyo, kama kutakuwa kuna kanuni
zinazozuia kuvunja kamati hii, jambo hili litakuwa gumu kutekelezwa na ikishindikana
kabisa nitamshauri tuonyane tu ndani ya baraza kwamba madiwani hatutakiwi kutoa
siri ya vikao vyetu vya kamati”, alisema.
No comments:
Post a Comment